Serikali yajipanga kutoa pesheni kwa wazee Tanzania

Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Lucy Nkya

Na Catherine Sungura, MOHSW, Lindi

SERIKALI imesema inaendelea kukamilisha taratibu zitakaowezesha utekelezaji wa suala la kutoa pensheni jamii kwa wazee ili liwe endelevu kulingana na mustakabali wa maisha ya wazee wa Tanzania. Kauli hiyo imetolewa leo mjini hapa na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Lucy Nkya kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya wazee duniani yaliyofanyika mkoani hapa kitaifa.
Alisema asilimia 4 tu ya wazee ndio wanaopata pensheni na asilimia 96 hawapati, hivyo Serikali inatambua hali hii na inathamini mchango wa wazee katika maendeleo ya nchi. “Suala la kutoa pensheni jamii ni la muhimu na ni njia pekee itakayowahikikishia wazee wote maisha bora, suala hili linahusisha gharama na linatakiwa kuwa endelevu hivyo Serikali inaendelea kuchukua hatua kutekeleza suala hili.
Dk. Nkya alisema Serikali inatekeleza masuala ya wazee kulingana na na sera ya taifa kwa kuchukua hatua mbalimbali zinazolenga kuhakikisha kuwa wazee wanaishi maisha yenye heshima kwa kuzingatia utu wao.
Aidha alisema pamoja na sera ya taifa ya wazee kuainisha masuala yanayowahusu wazee katika maamuzi yao na yale ya Kitaifa, sera hiyo inatakiwa kufanyiwa mapitio ili kukidhi mahitaji ya wazee kulingana na mabadiliko yanayotokea nchini.
Hata hivyo alisema mchakato wa kupitia sera ya taifa ya wazee itakapokamilika, Serikali itakamilisha taratibu za kutungwa kwa sheria itakayolinda haki ya wazee, “kwakuwa shughuli hizi zinahitaji umakini na tena kufanyika kwa awamu, nawasihi wazee mtoe ushirikiano kwa serikali na ushiriki wenu ni muhimu pale utakapohitajika.”
Kuhusiana na matibabu Naibu Waziri alisema Serikali imepitia mwongozo wa uchangiaji wa huduma za afya ya mwaka 2009/2010 ambapo mapendekezo ya namna ya kuboresha huduma za afya hasa makundi maalum yalitolewa ikiwemo kutoa huduma za afya bila malipo kwa wazee wote na si kwa wazee wasio na uwezo tu kama sera ya afya ya mwaka 2007 inavyoeleza. “Mwongozo huu bado upo katika ngazi muhimu za Serikali kwa ajili ya kuukamilisha, mara utakapokamilika utaanza kutumiaka” alisema.
Awali akisoma risala ya wazee kwa mgeni rasmi Mwenyekiti wa mtandao wa kinga ya jamii ya wazee Bi. Theresia Minja alisema wanaiomba Serikali kuweka utaratibu mahususi wa ufuatiliaji na kutathimini utekelezaji wa matibabu ya wazee kila baada ya miezi mitatu ili kupima utekelezaji wake kama ilivyo kwa sera nyingine zinazohusu mama na mtoto. Aidha, wazee wote waingizwe kwenye mifumo ya mifuko ya afya ya jamii kwa kuchangiwa na halmashauri za wilaya zao.

Kauli mbiu ya siku ya wazee duniaka mwaka huu ni “Miaka 10 ya uzindizi wa mpango kazi wa Madrid: Ongezeko la fursa na changamoto za uzee duniani”.Mpango kazi wa Madrid ulipitishwa na umoja wa mataifa mwaka 2002, ni mkataba wa kwanza kutambua umuhimu wa wazee katika kuchangia masuala ya uzee katika sera za maendeleo ya jamii zao na kuhitaji serikali kujumuisha masuala ya uzee katika sera za maendeleo ya jamii ya kiuchumi zikiwmo program za kupunguza umasikini.