Na Dotto Mwaibale
SAKATA la Julieth Daudi (19) mkazi wa Tabata Relini pamoja na ndugu zake kususia kuchukua mwili wa mtoto aliyejifungua kwa madai kuwa mtoto huyo hakuwa wake huku akidai kabadilishiwa na wauguzi wa Hospitali ya Amana, Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam baada ya kujifungua limechua sura mpya kufuatia wazazi hao kutaka kwenda kumuona Waziri wa Afya kufikisha kilio chao.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi nyumbani kwao Dar es Salaam, Daudi alisema tunahitaji kwenda kumuona Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kwa hatua zaidi kutokana na kitendo hicho walichofanyiwa na wauuguzi hao.
“Mimi pamoja na ndugu zangu tutakwenda kumuona waziri ili kumpelekea malalamiko yetu,” alisema Daudi.
Akizungumzia mkasa huo Daudi alisema alifika Hospitalini hapo Februari 2 jioni akiwa amesindikizwa na mama yake Veronica Lucas na shangazi yake Judith
Christopher.
“Nilipofika daktari aliponipima aliniambia kuwa hasikii mapigo ya mtoto isipokuwa ya kwangu hivyo alishauri siku iliyofuata nipate kipimo cha utrasaund lakini kabla ya
kipimo hicho nilijisia uchungu na kujifungua” alisema Daudi.
Daudi alisema baada ya kupita muda kidogo muuguzi aliyemzalisha alimfuata na kumueleza kuwa mtoto wake alikuwa amefariki na alipomuuliza alikuwa wa jinsia
gani muuguzi huyo alimweleza kuwa alikuwa hajui kama alikuwa wa kiume au wa kike.
Aliongeza kuwa wakati yupo wodini alimuona kijana mmoja aliyevalia koti la hospitali akiwa amembeba mtoto ambaye hakujua alikokuwa amempeleka.
Alisema baada ya kuambiwa mtoto wake amefariki aliomba aonyeshwe lakini hakuoneshwa tangu saa tatu asubuhi ambapo alilazimika kwenda kuomba simu kwa mlinzi wa hospitali hiyo na kuwajulisha ndugu zake walipofika nao waliomba kuonyeshwa mwili wa mtoto huyo bila mafanikio.
Shangazi wa Julieth Judith Christopher alisema baada ya kutokea tukio hilo walikwenda kumuona Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo ambaye aliitisha kikao baina ya ndugu pamoja na maofisa wengine wa hospitali hiyo ambacho hakikufikia muafaka baada ya ndugu hao kukataa kuuchukua mwili wa mtoto huyo wakidai si wa kwao.
Aliongeza kuwa mganga mkuu huyo aliwaeleza kuwa mtoto huyo alikuwa amefia tumboni baada ya mimba hiyo kuharibika na ndiyo sababu mtoto huyo alizaliwa akiwa
mfu.
“Wanafamilia tumegoma kuuchukua mwili wa mtoto huyo na maamuzi yaliyofikiwa ni kufanyika kipimo cha DNA” alisema Christopher.
Alipopigiwa simu Muuguzi Mkuu wa Hospitali hiyo, Beauty Mwambebule alisema hawezi kulizungumzia tukio hilo kwenye simu njia ya simu badala yake alimtaka mwandishi wetu kwenda hospitali kupata undani wa jambo hilo.