Mradi wa Africa Rising Kuzuia Upotevu wa Mazao

4B7A9628

Na; Ferdinand Shayo, Morogoro.
Asilimia 20 mpaka 40 ya mazao yanayovunwa na wakulima hasa mahindi hupotea kuanzia kipindi cha uvunaji mpaka kuhifadhi. kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo mbinu hafifu za uhifadhi wa mazao hayo.

Mazao ya Wakulima huanza kupotea yakiwa shambani kipindi cha uvunaji,usafirishaji ,kuanika na kuhifadhi.

Wakulima wengi wamekuwa wakitumia mbinu duni za kuhifadhi mazao yao na kujikuta wakipoteza kiasi kikubwa.

Wengine wamekuwa wakitumia madawa makali ya viwandani kwa kuhifadhia na yenye kemikali ambayo hubaki kwenye mazao na kusababisha madhara kwenye mwili wa binadamu ikiwemo magonjwa ya saratani.
Kutokana na changamoto hiyo mradi wa Africa RISING unaosimamiwa na Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo cha Kitropiki (IITA) kwa kushirikiana na wadau mbali mbali unatoa elimu kwa wakulima kuhusu kuzuia upotevu wa mazao hasa mahindi, jamii ya mikunde na karanga.

Pia unafanyauhimizaji wa matumizi ya mifuko ya kinga njaa maarufu kama “mifuko ya PICS” kwa kushirikiana na wasambazaji wa teknolojia hiyo rafiki kwa wakulima ambayo haihusishi matumizi ya kemikali za kuhifadhia mazao.

Mkulima hutakiwa kuhifadhi mahindi yake katika mfuko maalumu ambao haupitishi hewa na hauruhusu mdudu wa aina yoyote kupenya katika mfuko huo.

Wakulima wa Kilosa kutoka kikundi cha Kwimage kilichopo Kijiji cha Maguha wameeleza kunufaika na teknolojia hiyo ambapo awali kabla ya kutumia teknolojia hiyo walikuwa wakipoteza kiasi kikubwa cha mazao yao.

Andrew Chahunga ni Mkulima Anasema kuwa baada ya kupatia elimu juu ya kutumia mifuko hiyo wakulima waliamua kuhifadhi mahindi yao kama kikundi na baada ya miezi 6 waliyakuta mahindi yao yakiwa katika hali nzuri tofauti na yale yanayohifadhiwa kwa kutumia madawa ya viwandani.

“Kwa kweli tumetumia njia hii ya kuhifadhi mazao na imekuwa msaada mkubwa sana kwetu. Mahindi tuliyoyahifadhi ni salama kwa chakula kwenye familia zetu na hata kwenda masokoni kwa ajili ya kuuza” Alisema

Anaeleza kuwa uhifadhi huo umesaidia kuepukana na njaa katika kaya nyingi ambazo ni masikini na ambazo hutegemea kilimo kama njia ya kujipatia chakula pamoja na kipato.

Alex Mbigo, Mwenyekiti wa Kikundi cha Kwimage anasema kabla ya kutumia teknolijia hii mahindi yao yalikua yakiharibiwa vibaya na wadudu (kubunguliwa). Katika gunia moja lenye debe saba 7 huambulia debe tano 5 pekee huku madebe mawili yakiliwa na wadudu alieleza.

“Mradi wa Africa RISING kutoa mifuko ya kuhifadhia chakula umetufariji sana hivi sasa tunao uwezo wa kutumia mahindi hata kwa kusaga dona “

Fanuel Sinyagwa anaeleza kuwa teknolijia hiyo bado ilikua haijafika kijijini hapo ,mifuko hiyo inafanana na magunia yao ya asili kwa ujazo hivyo imekua rahisi kutumia teknolojia hiyo.

Licha ya Kutumia mifuko hiyo Changamoto tunayokutana nayo ni ukosefu wa maghala ya kuhifadhia chakula kwani upotevu mkubwa wa mahindi hutokea majumbani zaidi .

“Teknolojia hii ni rahisi haitumii gharama kubwa ,gharama yake ni mfuko na mfuko unaweza kuutumia kwa muda wa miaka mitatu na mahindi yako yakabaki salama” Alisema

Hellen Lezi ni Mwanakikundi wa Kwimage anaeleza kuwa mifuko hiyo inasaidia kuhifadhi chakula na kuepukana na njaa katika kaya .

Mtafiti Msaidizi wa Mradi wa Africa RISING Audifas Gaspar anasema kuwa licha ya juhudi zinazofanywa na serikali pamoja na mashirika binafsi bado mkulima anapoteza hadi asilimia 40% ya mazao yake tangu yanapokuwa shambani mpaka yanapovunwa ,wakati wakipakia kwenye vyombo vya usafiri ,upukuchuaji, kuanika na kuhifadhi.

Mifuko ya kinga njaa ni mkombozi wa Mkulima ambapo inaweza kupunguza upotevu sambamba na teknolojia nyingine za upukuchuaji na uanikaji kutoka asilimia 40 mpaka chini ya asilimia 3.

Amesema kuwa Mfuko huo unakuwa na matabaka mawili ya plastiki pamoja na salfeti ambazo zinapunguza uwezekano wa wadudu kushambulia mahindi.

Utumiaji wa madawa katika uhifadhi una changamoto nyingi ikiwemo dawa feki zilizopo sokoni na matumizi mabaya ya dawa hizo zinazoweza kuwa sumu kwa binadamu na kuleta athari.

“Sisi kama Wataalamu tunashirikiana na Wakulima juu ya namna bora ya kuhifadhi mazao yasiharibike,tunatoa elimu kwa njia ya vikundi vya wakulima” Alisema Audifas.

ferdinandshayo@gmail.com
0765938008