SERIKALI imezindua mwongozo wa mpango na usanifu wa ujenzi wa barabara zinazopitisha magari machache kwa lengo la kutoa maelekezo na kuwawezesha wahandisi wanaofanya usanifu wa barabara hizo kutumia gharama nafuu za ujenzi.
Akizungumza katika uzinduzi huo leo jijini Dar es salaam Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Eng. Joseph Nyamhanga amesema kuwa mwongozo huu utakuwa tiba na kuwezesha Serikali kujenga barabara nyingi na gharama nafuu.
“Ujenzi na ukarabati ya barabara zinazopitisha magari chini ya 300 kwa siku utakuwa wa gharama nafuu, kama tutatumia mwongozo huu kwani utasaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili barabara nyingi hususan za vijijini”, amesema Katibu Mkuu.
Amewataka wahandisi na Mafundi ujenzi kutumia mwongozo huo katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuweza kusaidia kazi na miradi mbalimbali ya barabara kuweza kufanyika kwa viwango vilivyo bora na gharama nafuu.
“Hakikisheni wahandisi na Mafundi ujenzi mnafuata mwongozo huu ipasavyo na kuanzia sasa uwe dira kwenu katika kazi zenu za kila siku”, amesisitiza Eng. Nyamhanga.
Ameongeza kuwa kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanywa Serikali imegundua uhitaji mkubwa katika mtandao wa barabara nchini ili kusaidia maendeleo ya kila mwananchi mijini na vijijini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Barabara katika Wizara hiyo Eng. Ven Ndyamukama amesema kuwa mwongozo huo unafananua namna ujenzi wa barabara hizo unavyokuwa ikiwemo kujenga kulingana na idadi ya magari yanayopita.
Ameongeza kuwa Mwongozo huo unaelekeza kutumia rasilimali chache zilizopo na kuhakikisha masuala ya mazingira katika maeneo yanayojengwa barabara hizo yatazingatiwa.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano