Na Mwandishi Wetu
ALAMA za bomoa bomoa (X) zinazowekwa kwa baadhi ya nyumba zilizojengwa kwenye eneo la hifadhi ya barabara limesambaa eneo kubwa nchini, yakiwemo maeneo ya miji midogo-zoezi ambalo endapo litatekelezwa huenda likawaumiza Watanzania wengi maeneo anuai.
Kwa mujibu wa uchunguzi ambao mtandao huu umeufanya hadi sasa katika mikoa ya Mara, Morogoro, Iringa, Mbeya, Kagera, Kilimanjaro, Arusha, Rukwa, Mwanza na Dar es Salaam umebaini majengo mengi binafsi, taasisi za Serikali na zisizo na Serikali yanaguswa na zoezi hilo.
Mazingira yanaonesha utekelezwaji wa zoezi hili utakuwa mgumu na huenda ukazua mgogoro mkubwa kati ya Serikali, Wananchi na taasisi nyingine kutokana na hali halisi ilivyo.
Uchunguzi umeonesha bomoa bomoa hiyo inagusa majengo makubwa ya taasisi mbalimbali nyeti zikiwemo za Serikali pamoja ja majengo ya kuabudu kiimani katika madhehebu mbalimbali.
Nyumba nyingi za wananchi wa kawaida zilizojengwa kisasa baadhi ya mikoa hiyo nazo zitatakiwa kubomolewa, hali ambayo huwenda ikazua mgogoro mkubwa kwa kada hiyo jambo ambalo limeifanya Serikali kuendelea kujiuliza kuridhia zoezi hilo kuanza mara moja, licha ya kwamba tayari majengo mengi yamewekewa alama ya ‘X’ tayari kwa kubomolewa.
Jana mtandao huu umebahatika kupita barabara ya kuelekea miji ya Gonja, Kisiwani, Ndungu Wilayani Same ambapo idadi kubwa ya nyumba za kisasa na za kawaida za wakazi wa pembezoni mwa barabara ya kuelekea miji hiyo zimekubwa na zoezi hilo.
Tayari Serikali imezuia kwa muda utekelezaji wa bomoa bomoa hiyo ikiangalia nini cha kufanya kabla ya kuendelea.