DC Hai Atoa Maelekezo kwa Mkurugenzi Juu ya Watumishi Wabadhilifu

Mkuu wa wilaya ya Hai, Gelasius Byakanwa akionesha sehemu ya nyaraka ambazo zinaonesha namna baadhi ya watumishi walivyoshiriki kufanya ubadhilifu wa fedha za madawati.

Mkuu wa wilaya ya Hai, Gelasius Byakanwa akionesha sehemu ya nyaraka ambazo zinaonesha namna baadhi ya watumishi walivyoshiriki kufanya ubadhilifu wa fedha za madawati.

 

Mkuu wa wilaya ya Hai, Gelasius Byakanwa akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Hai kuhusu ubadhilifu uliofanyika wakati wa zoezi la utengenezaji wa madawati. Kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Yahana Sintoo.
Baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Hai wakiwa katika kikao hicho.
Mkuu wa wilaya ya Hai,Gelasius Byakanawa (katikati) akiwa na katibu tawala wa wilaya hiyo, Upendo Wela (kulia) pamoja na Mkurugenzi wa Halamshauri ya wilaya hiyo Yohana Sintoo (kushoto).
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Hai, Yohana Sintoo akizungungunza wakati wa kikao hicho . 
 
Na Dixon Busagaga, Hai.
 
MKUU wa Wilaya ya Hai, Gelasius Byakanwa ametoa jukumu kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Yohana Sintoo la kuamua hatma ya watumishi wake watano wanaotajwa katika tuhuma za ubadhilifu wa fedha wakati wa zoezi la utengenezaji wa madawati.
 
Akiwa ndio mamlaka ya nidhamu kwa watumishi wa halmashauri hiyo, Mkurugenzi Sintoo ndiye mwenye maamuzi ya kuwasimamisha
kazi watumishi hao baada ya tume iliyoundwa na mkuu wa wilaya hiyo, Byakanwa kumaliza kazi yake ya uchunguzi dhidi ya watumishi hao na kubaini mapungufu kadhaa.
Akihitimisha taarifa yake wakati wa kikao na watumishi wa halmashauri hiyo, Byakanwa aliagiza taasisi ya kuzuia na
kupambana na rushwa (TAKUKURU) kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya watumishi hao akiwemo aliyekuwa kaimu Mkurugenzi, Mhandisi Kweka.
 “Mamlaka ya nidhamu ya watumishi wa Halmashauri ni mkurugenzi pamoja na baraza la madiwani ,lakini mwajiri ni ofisi ya katibu tawala mkoa, Ofisi hizi mbili ndizo zinazoweza kukaa na kuchukua hatua za kuzuia matukio au vitendo kama hivyo.” alisema Byakanwa.
 “Niishauri ofisi ya Katibu tawala mkoa wa Kilimanjaro pamoja na ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Hai  ambayo ndio mamlaka ya nidhamu kwa watumishi hao kupima kuhusu hatua za kuchukua dhidi ya watumishi hawa,” aliongeza Byakanwa.
Mkuu huyo wa wilaya alisema tuhuma zinazowakabili watumishi hao, majina yao tumeyahifadhi kwa sasa ni pamoja na kupitisha barua ya malipo bila kujiridhisha kama kuna mkataba wa kutengeneza madawati na kufanya malipo ya fremu za madawati badala ya madawati.
 Tuhuma nyingine inaihusu timu ya ukaguzi  iliyokiri kukamilika kwa kazi bila ya kuonesha kama walipokea madawati au walienda kukagua kazi ya mzabuni  licha ya mzabuni kuomba malipo ya fremu za madawati badala ya Madawati kamili. Ofisi ya elimu msingi, ofisi ya mkurugenzi, ofisi ya Mhasibu wa Halamshauri na kitengo cha manunuzi pia zinatuhumiwa kushindwa kubaini nyaraka zilizowasilishwa na mzabuni endapo zilikuwa ni kwa ajili ya fremu za Madawati badala ya  Madawati kamili.
Katika kikao hicho kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo Byakanwa alisema kampuni iliyopewa zabuni ya
kutengeneza madawati ni ya Ujenzi na haijawahi kufanya kazi ya kutengeneza madawati, kuwa na karakana wala  vifaa vya uselemala. 
Byakanwa alisema kwa malipo yaliyofanyika Halmashauri ilipoteza zaidi ya sh Mil 12 huku akishangazwa na hatua ya mmoja wa watumishi wanaotuhumiwa kuomba malipo badala ya mzabuni.
Akionyesha namna watumishi hao walivyokiuka taratibu Byakanwa alisema taarifa ya uchunguzi inaonyesha Halmashauri iliunda
timu ya ukaguzi ambayo katika cheti cha ukaguzi na mapokezi ya bidhaa kinaonyesha bidhaa au madawati yalipelekwa, Julai 16, 2016, siku 12 tangu siku ya mkataba na mzabuni.
“Mmoja w wajumbe wa kamati hiyo ya ukaguzi alikuwa ni mjumbe wa kamati ya kuratibu zoezi la Madawati ,alikuwa na jukumu la
kusambaza mbao kwa wazabuni na alikuwa anajua kuwa hajapeleka mbao za kutosha kwa mzabuni, katika maelezo yake mbele ya tume anakiri kuwa mzabuni hajamaliza kazi kwa sababu Halmashauri haijampa mbao.” alisema Byakanwa.
Alisema mzabuni aliieleza tume kuwa anadaiwa madawati 246 na halmashauri na kuwa amekamilisha kutegeneza madawati
154 na ueleza kua alishindwa kukamilisha kutokana na kukosa mbao kutoka halmashauri.
“June 9,2016 malipo ya Sh Mil 19.2 yakalipwa kwa ajili ya fremu za madawati siyo Madawati.Vocha ya malipo ikasainiwa
na DT na kuandaliwa na mtumishi mwingine (jina tunalo) ikakamilisha mchezo.”alisema Byakanwa.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kufanya hivyo ilikuwa ni kinyume cha taratibu za malipo kwa kuwa wahusika walipaswa kujiridhisha na nyaraka walizokuwa wakitumia ,kwa nini mzabuni aliamua kudanganya Halmashauri.
Byakanwa aliishauri ofisi ya Katibu tawala mkoa wa Kilimanjaro pamoja na ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya
Hai  ambayo ndio mamlaka ya nidhamu kwa watumishi hao kupima kuhusu hatua za kuchukua dhidi ya watumishi hao.
Kwa upande wake mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Hai,Yahana Sintoo alisema licha ya kwamba amefika wakati zoezi la
uchunguzi lina kamilika bado atafanyia kazi taarifa hizo kwa umakini mkubwa ili kujiridhisha na utendajji kazi wa watumishi wa halmashauri hiyo.