Ridhiwani Kikwete na Kauli ya Matumaini kwa Wasanii Tanzania

Ridhiwani Kikwete (kulia) akiwa katika uzinduzi wa video ya mwanamuziki Belle 9

Ridhiwani Kikwete (kulia) akiwa katika uzinduzi wa video ya mwanamuziki Belle 9

MBUNGE wa Jimbo la Chalinze, Mh. Ridhiwani Kikwete amesema anatamani kuona kazi za wasanii wa Tanzania zinatambuliwa na wasanii hao kupata faida juu ya kazi wanazofanya. Ameongeza kuwa anapenda kuona Wanamuziki wa Tanzania wakifanya vizuri na huku wakinufaika na kazi zao na kukuza soko la Muziki huo Kimataifa.

Mbunge huyo amesema hayo alipokua Mgeni rasmi katika uzinduzi wa Video ya mwanamuziki Belle 9 ya muziki wake mpya unaoitwa Give It To Me ambao amemshirikisha mwanamuziki G Nako.

Akizungumza katika Uzinduzi huo, amesema anapenda kuona muziki wa Tanzania na wasanii wake kazi zao zikitambulika na pia waone faida ya kazi wanayoifanya. Katika Uzinduzi huo amesema amejitoa kumsaidia Msanii Belle 9 kutokana na uwezo wake wa Kuimba na kipaji alichonacho.

Ameongeza kuwa yeye ni Mbunge kijana anayetaka kuona wasanii Watanzania kazi zao zinatambuliwa na kuona faida ya kazi wanazofanya.

Aidha ameupongeza uongozi mzima wa Vitamin Music kwa kufanikisha tukio hilo na kusema wimbo wa Give It To Me bila shaka, unaongeza idadi ya nyimbo zitakazokuwa maarufu kwenye Klabu za Tanzania. Ameeleza kwamba anafurahi kuona wasanii wanaanza kuondoa ile imani kuwa Bongo Flava ni muziki wa kusikiliza zaidi, na kusema ndio maana unakuta hafla mbalimbali ikiwemo Harusi au mashindano kama Miss Tanzania, zinajaa Playlist za nyimbo za Nigeria.

Aidha amepongeza Wanamuziki kwa hatua yao ya kufikiria kuweka ‘fusion’ za muziki wa Asili kwenye nyimbo zao ili kuzipa ‘Utanzania’ unaoliliwa kila siku. Amesema Wimbo huo wa Belle 9 una Video nzuri na anaamini itamfikisha Belle sehemu ambazo bado hajafika.