MKURUGENZI Mtendaji wa mtandao wa JamiiForums, Maxence Melo amenyimwa dhamana ya polisi kwa madai ya “amri kutoka kwa wakubwa.” Taarifa zinaeleza kuwa Maxence aliitikia mwito wa Polisi – Kanda Maalum ya Dar es Salaam, leo asubuhi, lakini alipofika Kituo Kikuu cha Kati cha Polisi, alizuiliwa na polisi.
Akiwa ameongozana na mwanaharakati wa kutetea uhuru wa mawasiliano na mhariri, Simon Mkina na mwanasheria, Nakazael Tenga, Maxence alikosa dhamana kwa maelekezo kuwa iliamuriwa na wakubwa “alale” kituoni hapo hadi kesho. Mwanasheria Tenga alishangazwa kwa hatua hiyo ya Jeshi la Polisi na kueleza kuwa siyo haki kwa mtuhumiwa kunyimwa dhamana.
Maxence atafikishwa mahakamani kesho kujibu mashitaka ya kuzuia upepelezi wa makosa ya mtandao. Kwamba amekuwa akishindwa kutoa ushirikiano kwa polisi wanapohitaji kupewa taarifa za wachangiaji wa mtandao wa JamiiForums. Atafikishwa Mahakama ya Wilaya ya Ilala kesho saa 2.30 asubuhi.
Maxence alifika Polisi saa 6.17 na baada ya saa moja, aliamuriwa kuingia selo, huku waliomsindikiza wakielezwa kuondoka eneo la polisi.
JamiiForums imekuwa na msimamo wa kutotoa habari za wachangiaji wake kwa yeyote, kwani kufanya hivyo ni kuingialia uhuru na faragha ya wateja wake.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2006, msingi mkuu wa mtandao wa JamiiForums umekuwa kulinda faragha ya watumiaji wake. Watumiaji wa mtandao wa JamiiForums wako huru kuweka mijadala, kuanzisha mijadala, kuchangia chochote pasipo kuvunja sheria za nchi au kuhatarisha usalama wa taifa.
Kampuni ya Jamii Media, inayoendesha mitandao ya JamiiForums.com na FikraPevu.com imejijengea heshima na umaarufu kwa muda mrefu kutokana na namna inavyoendesha na kusimamia shughuli zake ambazo kwa kiwango kikubwa. Mtandao wa JamiiForums ni mtandao mkubwa wa Kiswahili kwa Afrika Mashariki na duniani ukiwa na wasomaji wasiopungua Milioni 2.5.