Amani ya Tanzania yamvuta Balozi wa Papa Benedict 16

Balozi wa Baba Mtakatifu nchini Tanzania, Mhashamu Askofu Mkuu Joseph Chennoth.

KIONGOZI wa Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Benedict wa 16 ameeleza kufurahishwa na kuridhishwa kwake na amani, utulivu na uvumilivu wa kidini ulioko baina ya dini mbalimbali nchini na baina ya Watanzania wenye imani mbalimbali za kidini katika Tanzania.

Pamoja na kutaka kujua hasa nini siri ya mafanikio ya utulivu na uvumilivu huo wa kidini katika Tanzania, Baba Mtakatifu pia amewapongeza viongozi wa nyanja na sekta mbalimbali katika Tanzania kwa kudumisha uvumilivu huo na kuwataka kuendeleza kushikilia siri ambayo imedumisha utulivu huo kwa miaka 50 tokea uhuru.

Msimamo huo wa Papa Benedict wa 16 umeelekezwa Septemba 29, 2011, na Balozi wa Makao Makuu ya Baba Mtakatifu ya Vatican katika Tanzania, Mhashamu Askofu Mkuu Joseph Chennoth wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Ikulu, Dar es Salaam.

Mhashamu Askofu Mkuu Chennoth alikuwa anamuaga Rais Kikwete baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi wa Vatican katika Tanzania. Askofu Mkuu Chennoth amekaa nchini miaka sita ikiwa sehemu ya miaka 15 ambako ameiwakilisha Vatican katika nchi mbalimbali za Afrika.
Balozi Chennoth ambaye aliwasili nchini Agosti 22, mwaka 2005, na kuwasilisha hati zake za utambulisho siku tisa baadaye, Septemba Mosi, mwaka huo huo, anahamishiwa Japan.
Katika mazungumzo kati ya viongozi hao, Balozi Chennoth amemwambia Rais Kikwete: “Siku zote Baba Mtakatifu amekuwa anaulizia juu ya siri ya mafanikio ya uvumilivu wa kidini katika Tanzania. Kwa hakika, Baba Mtakatifu anatambua hali hii, anawapongeza viongozi wa Tanzania kwa kulisimamia na pia anaombea hali hii iendelee kuwepo katika Tanzania.”

Balozi Chennoth pia amemwambia Rais Kikwete kuwa kiongozi wa kweli kweli wa dini huhubiri amani, umoja na mapenzi na wala siyo mifarakano na mapigano.

Balozi pia amesifia ushirikiano uliopo katika Tanzania kati ya viongozi wa dini na wale wa siasa. “Sisi siyo washindani, siyo wapinzani. Sisi ni wabia na washiriki katika shughuli za kuwahudumia wananchi na kuwafikishia huduma za kijamii. Tunashirikiana katika utoaji elimu, katika utoaji huduma za afya na huduma nyingine za kiroho na kimwili. Kwa kweli imekuwa ni faraja yangu kubwa kutumikia katika nchi hii yenye historia ya kutukuka duniani, nchi ya Mwalimu Kambarage Nyerere.”

Rais Kikwete amempongeza Balozi huyo kwa kukuza uhusiano kati ya Tanzania na Vatican katika kipindi chake cha uwakilishi akisema, “umesaidia sana katika kuimarisha uhusiano kati ya Vatican na nchi yetu, kati ya umoja wa Kikatoliki duniani na wananchi wetu. Tunakushukuru sana.”

Rais Kikwete pia amesifia uhusiano ulioko kati ya Serikali yake na Kanisa Katoliki na kuwataka viongozi wa kisiasa na kidini kukumbuka kuwa wao wanayo dhamana kubwa ya kuendeleza uhusiano huo na pia kudumisha uvumilivu wa kidini katika Tanzania.

“Ni wajibu wetu sisi viongozi wa kisiasa na viongozi wa dini kuhakikisha kuwa nchi yetu inaendelea kuwa ya amani na tunaendelea kuishi kwa namna hii ya kuvumiliana kidini, kuoleana na kubakia ndugu. Jukumu hili liko mikononi mwetu. Tukivuruga utulivu huo tutakuwa tumeivuruga nchi yetu kwa namna ya kudumu hatutaupata tena utulivu huo kwa sababu ni vigumu sana kuutengeneza upya.”

Rais Kikwete pia ametumia nafasi ya mazungumzo hayo kumkumbusha Balozi Chennoth kuhusu mwaliko wake ambao aliutoa kwa Baba Mtakatifu wakati alipotembelea Vatican mwaka 2008. “Nilimpa mwaliko Baba Mtakatifu wakati tulipokutana Vatican wakati wa ziara yangu aliponialika nimtembelee na baada ya hapo tulipokutana mjini Napoli. Bado Wakatoliki wa Tanzania na Watanzania kwa jumla wanaendelea kumsubiri.”