Balozi wa Vatican Tanzania atoa pole Zanzibar

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein (kushoto) akisalimiana na Balozi wa Baba Mtakatifu nchini Tanzania, Joseph Chenoth

Na Rajab Mkasaba, Ikulu-Zanzibar

VATICAN imesema imeguswa na msiba mkubwa uliosababishwa na kuzama kwa meli ya Mv. Spice Islander na kutoa mkono wa pole kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein huku ikieleza kufarajika na namna ya uhuru wa kuabudu unavyoendelezwa nchini.

Hayo yalielezwa na Balozi wa Vatican nchini Tanzania, Joseph Chenoth aliyefika Ikulu mjini Zanzibar jana kwa ajili ya kuaga na kufanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein kutokana na na kumaliza muda wake wa kazi hapa nchini.

Katika maelezo yake Balozi Chenoth alimueleza Dk. Shein kuwa Vatican inatoa mkono wa pole kufuatia ajali hiyo kwani inatambua kuwa ni ajali mbaya ambayo haijawi kutokea hapa Zanzibar na kuwataka Wazanzibari na Watanzania wote kwa jumla kuwa pole.

Balozi Chenoth alisema kuwa tokea kutokea kwa msiba huo ibada na maombi mbali mbali yamekuwa yakifanywa kwa ajili ya kuwaombea marehemu pamoja na wale wote waliopata majeraha ili wapone haraka.

Pamoja na hayo, Balozi Chenoth, alisema kuwa Vatican itaendeleza uhusiano na ushirikiano wake na Zanzibar na kueleza kufarajika kwake na uhuru wa kuabudu uliopo hapa nchini pamoja na umoja na mshikamano wa hali ya juu.

Alisema kuwa anajivunia na hatua kubwa zilizofikiwa hapa nchini katika kuendeleza amani na utulivu uliopo ambao unatokana na kuimarishwa kwa uwepo wa uhuru wa kuabudu ambao nao umechangia kwa kiasi kikubwa kufikia hatua hiyo.

Balozi huyo wa Vaticana alisema kuwa juhudi hizo zimeanza kuchukuliwa tokea uongozi wa Marehemu Mzee Abeid Amani Karume na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kuendelea hadi hivi leo ambapo heshima katika uhuru wa kuabudu imepewa kipaumbele.

Sambamba na hayo, Balozi Chenoth alitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar kutokana na uchaguzi uliokuwa huru na wa amani na utulivu ambao umeijengea sifa kubwa Zanzibar Kitaifa na Kimataifa.

Pia, alitoa pongezi kwa wananchi wa Zanzibar kwa kuendeleza amani na utulivu huo na kueleza kuwa hatua hiyo ni miongoni mwa juhudi za kuipelekea Zanzibar kupata mafanikio makubwa.

Balozi Chenoth alisema kuwa anathamini uhusiano na ushirikiano mwema uliopo kati ya Zanzibar na Vatican na kueleza matumaini yake makubwa ya maendeleo kwa Zanzibar kutokana na uongozi wa Dk. Shein kiongozi ambaye alieleza kuwa ni mwenye uzoefu mkubwa wa uongozi na juhudi pamoja na maarifa katika kuongoza.

Nae Rais Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa kwa niaba ya wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla anapokea mkono wa pole kufuatia msiba huo mkubwa na kumueleza juhudi zilizochukuliwa na serikali zote mbili pamoja na wananchi katika kukabiliana na tukio hilo.

Dk. Shein alimueleza Balozi huyo wa Vatican kuwa Zanzibar ina historia kubwa ya uwepo wa dini tofauti hapa nchini ambapo ushahidi wake upo mpaka leo hii ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa nyumba za ibada,skuli za Msingi na Sekondari zilizojengwa wakati huo na mambo mengineyo.

Akieleza historia kwa ufupi juu ya uwepo wa uhusiano wa kidini hapa nchini Dk. Shein alisema kuwa hatua mbali mbali zimeanza tokea mnamo miaka mingi iliyopita ambapo hata wafalme waliotawala Zanzibar wakati huo waliwakaribisha wafusi wa dini nyengine hapa Zanzibar kwa ajili ya kuendeleza dini zao.

Dk. Shein alieleza kuwa mbali ya hatua hizo Katiba pia, imeruhusu uhuru wa kuabudu kwa kila mmoja na dini yake ambapo pia, alitoa shukurani kwa kiongozi huyo kwa kuiwakilisha vyema Vatican katika kipindi chote cha miaka sita aliyofanya kazi zake hapa nchini.

Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa mbali ya mashirikiano mbali mbali yaliopo kati ya Zanzibar na Vatican ipo haja pia kuzidisha uhusiano katika sekta ya elimu kwa kuvishirikisha Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar na vile Chuo Kikuu cha Vatican.