Sababu za Kuanzishwa Muswada wa Sheria za Huduma za Habari 2016

 

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye akizungumza.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye akizungumza.

Na Daudi Manongi, MAELEZO
SERIKALI kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo limefanya mchakato wa upatikanaji wa Sheria ya Huduma za Habari ambao umekuwa ni kilio kikubwa kwa wanahabari kwa zaidi ya miaka 20 na sasa uko mbele ya kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii ukikaribisha maoni kutoka kwa wadau mbalimbali wa sekta ya Habari ambapo mpaka sasa asilimia 90 ya maoni yamepokelewa.
Muswada huu wa Sheria za Huduma za Habari wa 2016 umelenga kuboresha taaluma ya uandishi wa Habari nchini na kuifanya kuwa rasmi mbele ya Jamii Muswada huu unapendekeza kutunga Sheria ya Huduma za Habari kwa madhumuni ya kuweka utaratibu wa kisheria katika tasnia ya habari, kuunda Bodi ya Ithibati ya Wanahabari, kuunda Baraza Huru la Habari, kushughulikia masuala ya kashfa, makosa yanayohusiana na utangazaji na masuala yanayohusiana na hayo.
Muswada huu umegawanyika katika Sehemu Nane. Sehemu ya Kwanza inahusika na masharti ya ambayo ni jina la Sheria, tarehe ya kuanza kutumika, matumizi na tafsiri ya misamiati na maneno yaliyotumika.
Sehemu ya Pili inahusika na Idara ya Habari kuwa Masemaji Mkuu wa Serikali, majukumu ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari, aina za umiliki wa vyombo vya habari, inatoa wajibu kwa vyombo vya habari kutoa habari kwa Umma na Serikali na pia inaainisha wajibu wa vyombo vya habari binafsi kutoa habari na kulinda maadili ya kitaaluma ya vyombo vya habari, utoaji leseni kwa magazeti, ufutwaji wa leseni na utaratibu wa kutoa malalamiko.
Sehemu ya Tatu inamaanisha masharti yanayohusu uanzishwaji wa Bodi ya Ithibati ya Wanahabari, muundo wa Bodi ya Ithibati, majukumu ya Bodi, mamlaka ya Bodi, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi, majukumu ya Mkurugenzi Mkuu, watumishi wa Bodi, uthibitishaji wa wanahabari, Kitambulisho cha Wanahabari, Mfuko wa Mafunzo ya Wanahabari na vyanzo vya fedha za Mfuko.
Sehemu ya Nne ina masharti yanayohusu uanzishwaji wa Baraza Huru la Habari, uanachama wa Baraza, majukumu ya Baraza, mwenendo na mikutano ya Baraza, mamlaka ya Baraza, majukumu ya Katibu wa Baraza na kuondolewa kwa Katibu wa Baraza. Vile vile, Sehemu hii inaipa Baraza mamlaka ya kushughulikia malalamiko dhidi ya machapisho. Mtu asiyeridhika na uamuzi wa Baraza anaweza kukata rufaa Mahakama Kuu.
Sehemu ya Tano inahusika na masuala ya kashfa Sehemu hii inatoa ufafanuzi endapo jambo lolote litachapishwa na kutangazwa na mtu na kusababisha kuharibu sifa ya mtu au kuchafua jina lake; mtu huyo atakuwa ametenda kosa kwa mujibu wa Sheria. Aidha Sehemu hii imeanisha utangazaji wa mambo yenye kashfa ambayo yanaruhusiwa ikiwa mambo hayo yatatangazwa na Rais Serikali au Bunge au jambo lolote litakalotangazwa mahakamani wakati wa kusikilizwa shauri au kutangaza jambo lolote kwa mujibu wa Sheria.
Sehemu ya Sita inaainisha masharti yanayohusu masuala ya fedha za Bodi na vyanzo vya mapato ya Bodi. Aidha, makadirio ya bajeti ya Bodi, utoaji wa taarifa za fedha, vitabu vya fedha vya Bodi pamoja na ukaguzi wake vimewekewa masharti. Sheria ya Huduma za Habari.
Sehemu ya Saba inahusu makosa mbalimbali ambayo yanahusu vyombo vya habari. Sehemu hii imeainisha makosa dhidi ya utangazaji wa habari ambao umepigwa marufuku, habari za kuchochea uasi, makosa ya uchochezi, utangazaji wa habari za uongo au za kutia hofu na woga kwa jamii. Aidha, makosa yanayotendwa na mashirika au kosa litakalotendwa na mtumishi anayemwakilisha mwajiri yameainishwa na kuwekewa adhabu.
Sehemu ya Nane inahusika na masuala ya jumla ambapo inapiga marufuku uingizaji wa machapisho ambayo hayana manufaa kwa umma. Aidha inampa mamlaka Mkurugenzi wa Huduma za Habari, afisa polisi au afisa yeyote muidhiniwa kukamata chombo chochote kinachoendeshwa kinyume na Sheria. Vile vile, Sehemu hii inaainisha masharti yanayompa mamlaka Waziri kutengeneza kanuni kwa ajili ya uendeshaji bora wa Sheria hii na uanzishwaji.