Benedict Liwenga- WHUSM
WADAU wa Habari wameisifu Serikali kwa kuundaa na kuwasilisha Bungeni Muswada wa Sheria ya Huduma za Jabari.
Wamesema ni jambo ambalo lilikuwa limesubiriwa kwa muda mrefu tangu mchakato ulipoanza miaka ya 80 na baadaye kuzimika halafu na kurudi tena miaka ya hivi karibuni hususani mwaka juzi na mwaka jana 2015.
Akiongea kupitia kituo kimoja cha cha Televisheni nchini jana, Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Jamhuri na Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini, Bw. Deodatus Balile amesema amefurahishwa sana na Muswaha huu kuwataka wanahabari kujiendeleza kitaaluma jambo ambalo amesema ni muhimu katika taaluma yoyote.
“Kwa kweli kuhusu Mwandishi wa habari kusoma au kuwa na digrii, hili naliunga mkono, inabidi waandishi wasome na kama hawataki kusoma basi wajaribu ujinga”, alisema Balile.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Hassan Abbas amesema kuwa Muswada huu ni muhimu kwa wanahabari na taaluma ya habari kwa ujumla kwani ni kwa mara ya kwanza katika Tanzania uandishi wa habari unaenda kuwa taaluma.
“Nipende kuwaasa wana taaluma wenzangu kuusoma Muswada huu na kutoa maoni badala ya kulalamika kwani sisi ndiyo tunaoielewa zaidi taaluma ya habari, hivyo maoni yetu ni muhimu”, alisema Abbas.
Abbas aliongeza kuwa, Muswada huo utafanya uandishi wa habari kuwa taaluma inayoheshimika na utaanzisha Baraza Huru la Habari na Bodi ya Ithibati ya wanahabari, mambo ambayo yamekuwa yakipiganiwa na wanahabari. Hivyo Muswada huu ni wa manufaa kwa wanahabari.
Akiongea katika ziara maalum aliyofanya Mkurugenzi wa MAELEZO katika ofisi za Majira, Mhariri Mtendaji wa Majira, Bwana Emmnanuel Mbuguni alisema kwamba amefurahishwa na kipengele cha wanahahabari kusoma ili kuongeza weledi katika kazi yao. Hivyo, amesema kwa jinsi hiyo anakubaliana na Muswada huo na akaahidi kutoa maoni yake zaidi kupitia barua pepe ya Bunge.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari umewasilishwa Bungeni mwezi Septemba mwaka huu na baadaye wadau wakaruhusiwa kutoa maoni yao kwenye muswada huo kabla ya kusomwa kwa mara ya pili mapema mwezi ujao yaani Novemba.