WAFUNGWA wapatao 2,747 wa Kenya ambao walikuwa wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa sasa wamebadilishiwa adhabu na sasa hawata nyongwa tena. Kwa mujibu wa taarifa kutoka Kenya wafungwa hao sasa watafungwa kifungo cha maisha badala ya kuuwawa.
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ametengua hukumu hiyo ya kifo na sasa wafungwa hao 2,747 watatumikia hukumu ya kigungo cha maisha wakiwa gerezani. Wafungwa wengi ambao wamekuwa wakihukumiwa kunyongwa hadi kufa nchini Kenya hukumu hiyo imekuwa haitekelezwi tangu miaka ya 1980.
Pamoja na hayo watetezi wa haki za binadamu wamekuwa wakipigania kuondolewa kwa hukumu hiyo, huku baadhi ya wafungwa nao wakilalamika kwamba hakuna tofauti ya hukumu ya kifo na kifungo cha maisha jela kwani mfungwa huwa anaishi jela hadi kifo chake.
Wakati huo huo, Rais Kenyatta amewasamehe wafungwa 102 waliokuwa wakitumikia vifungo mbalimbali virefu. Hivi karibuni pia alikuwa amewaachilia huru wafungwa takriban 7,000 wa makosa madogo madogo au waliokuwa wanakaribia kumaliza kutumikia vifungo vyao, na ambao walikuwa wameonyesha dalili za kubadilisha tabia tangu waanze kutumikia vifungo vyao.