UTAFITI uliofanywa na shirika la Railway Children Africa mkoani mwaka jana umebaini kuwa idadi kubwa ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi mitaani wamenyanyaswa kingono.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Shirika la Railway Children, Bw. Pete Kent alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kubainisha matokeo ya utafiti juu ya watoto wa mitaani mkoani Mwanza.
Alisema utafiti umebaini kuwa, asilimia 100 ya watoto wa mitaani wamewahi kunyanyaswa kimwili kwa vitendo au hata kwa maneno, huku ukionesha asilimia100 ya wasichana na 25 ya wavulana wakidhalilishwa kijinsia.
“Watoto na familia zilizoathiriwa na ukatili mara nyingi hutengwa na kunauwezekano wa kutonufaika na mipango endelevu na badala yake wanahitaji huduma zaidi za kiushauri ili kutibu majeraha yaliyotokana na ukatili katika familia zao,” alisema Mkurugenzi Kent.
Aidha Afisa Mradi wa Shirika la Railway Children Africa, Adam Kaombwa aliongeza kuwa utafiti huo ulibaini jumla ya watoto 1940 wanaishi na kufanya kazi mitaani katika Jiji la Mwanza, ikiwa ni ongezeko la asilimia 25 ukilinganisha na tafiti za nyuma.
Alisema utafiti umebaini ndani ya miezi 12, idadi ya wasichana wanaofanya biashara ya ngono imeongezeka kwa asilimis 229, huku ongezeko kubwa likiwa ni la wasichana wenye umri wa kati ya miaka 11 hadi 14.
“Idadi ya wasichana wanaofanya biashara ya ngono ni 418, na kati ya hao 218 ni wenye umri chini ya miaka 18. Pia kuna hali ya kupungua kwa asilimia 40 ya watoto wa mitaani wenye umri kati ya miaka 0-14 kwa kipindi cha ya miaka mitatu – kwa walengwa wetu wakuu,” alieleza Kaombwa.
Alisema pamoja na hayo shirika linatambua juhudi za serikali ya Tanzania katika kutoa huduma, msaada na ulinzi kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na kuwepo kwa Mpango wa Taifa wa Kukomesha Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto na hadhi ya Tanzania kama nchi ya mfano katika Ubia wa Kimataifa wa Kukomesha Ukatili dhidi ya Watoto.
Hata hivyo ameipongeza kwa jitihada dhahiri za kuwepo kwa dhamira ya kweli ya kisiasa katika kubadili hali ya watoto wote wanaoishi katika mazingira magumu, wakiwemo watoto mitaani.
Pamoja na hayo ili kukabiliana na ongezeko la watoto wanaoishi katika mazingira magumu, hatarishi na wapweke mitaani shirika la Railway Children Africa limeandaa kongamano la kimataifa la ‘Kuvunja mzunguko’ linalotarajiwa kufanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Benki kuu ya Tanzania Novemba 17- 18 mwaka huu.
Kongamano la kuvunja mzunguko ni kwa mtu yeyote anayeweza kufanya kazi ili kubadilisha maisha ya watoto wa mitaani-kushikamana popote duniani, ikiwa ni pamoja na wale wanaofanya kazi katika jamii moja kwa moja, kubuni mipango ya mashirika yasiyo ya kiserikali, watunga sera, bajeti au watafiti.
Bw. Kent aliongeza kuwa kongamano hilo litatoa fursa kwa wajumbe zaidi ya 250 kushirikiana, kujifunza na kupata uelewa mkubwa wa mikakati iliyothibitika ya kuvunja mzunguko wa ukatili kwa familia dhidi ya watoto wanaoishi mitaani.