Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk. Hassan Mshinda, akizindua utafiti huo katika Kituo cha Utafiti cha Makutupora mkoani Dodoma juzi.
Watafiti kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), na Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi wakiwa tayari kwa upandaji wa mbegu hizo katika Kituo cha Utafiti cha Makutopora mkoani Dodoma.
Mratibu wa Jukwaa la Bioteknolojia Tanzania (OFAB), Philbert Nyinondi, akishiriki kupanda mbegu hizo.
Mshauri wa Mradi wa WEMA, Dk. Alois Kullaya (kushoto) na Meneja mradi huo Mr Silvester wakishiriki kwenye upandaji wa mbegu hizo.
Watafiti wakichoma masalia ya vifungashio vya mbegu za mahindi kama sheria ya GMO inavyoelekeza baada ya zoezi hilo.
Na Dotto Mwaibale
KWA mara ya kwanza Tanzania imeanza kufanya utafiti wa mbegu ya mahindi meupe kwa kutumia teknolojia ya uhandisi jeni (GMO) ambao utachukua takriban miaka mitatu ili kupata matokeo ya mbegu nzuri itakayostahimili mabadiliko ya hali ya hewa ambayo imekuwa changamoto kubwa kwa wakulima.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dk. Hassan Mshinda alisema kuanza kwa utafiti huo ni hatua nzuri kwa nchi katika kuinua kilimo nchini.
Alisema utafiti huo ambao unafanyika katika nchi tano za Afrika, kwa hapa nchini unafanyika katika kituo cha Makutopora mkoani Dodoma na kuwa nchi hizo nyingine ni Kenya, Uganda, Africa ya Kusini na Msumbiji.
Mtafiti na Mshauri wa mradi wa mahindi yanayostahimili ukame ( WEMA) Dk. Alois Kullaya, alisema Tanzania ilikuwa ikifanya tafiti katika hatua ya maabara, na sasa kwa mara ya kwanza wapanda kwenye mazingira halisia. ” Ni kweli tarehe tano ya mwezi huu, tulipanda mahindi meupe katika hatua ya utafiti kwenye mazingira. Tunataka tujiridhishe na uwezo wa mahindi hayo katika kustahimili ukame”. Matokeo ya utafiti huu, utatoa nafasi kwetu kama watafiti na viongozi wetu kufanya maamuzi yenye tija kwa taifa badala ya kuwa watazamaji na kushambikia marumbano tusiyofahamu chanzo chake” alisema Kullaya.
Mtafiti Kiongozi wa masuala ya bioteknolojia kutoka Costech Dk. Nicholas Nyange aliishukuru serikali kwa kuruhusu watafiti wake kuweza kufanya majaribio ya uhandisi jeni hapa nchi. Hii ni hatua nzuri katika nchi yoyote inayoamini katika maendeleo ya sayansi na teknolojia.
“Tumekuwa tukitishiwa kama watoto Usiguse GMO utakufa, wakati nchi nyingine wanazalisha nakufanya biashara. Tunafanya biashara kubwa na India, China, Marekani na Afrika ya Kusini, na hawa wote wanatumia teknolojia ya uhandisi jeni”.
“Tufanye utafiti, tuone kama tutakufa kweli au tutatoka kimasomaso” aliongeza Nyange kwa tabasamu.
Itakumbukwa kuwa Mradi wa WEMA hadi sasa umezalisha mbegu 11 za mahindi kwa njia za kawaida. Na baadhi ya mbegu hizo zimeingia sokoni mwaka huu kwa bei ya kawaida. Hivyo, uzalishaji wa Mahindi ya GMO itakuwa ni hatua mbele katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi.