Mke wa Rais Obama Kujadiliana na Wasichana Watanzania

Bi. Michelle Obama

Bi. Michelle Obama

 

WASICHANA 25 kutoka nchini Tanzania wanatarajiwa kufanya majadiliano ya moja kwa moja na mke wa Rais wa Marekani, Bi Michelle Obama wiki ijayo.

Wasichana hao ni miongoni mwa wasichana wa nchi tatu watakaoshiriki majadiliano hayo yenye lengo la kumuwezesha mtoto msichana katika masuala mbalimbali na upatikanaji wa fursa.

Majadiliano hayo ni tukio litakalofanywa na Shirika la Plan International Tanzania na yatafanyikia katika ubalozi wa Marekani, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Msichana Duniani tarehe 11 Oktoba, 2016. Mkurugenzi Mkazi wa Plan International Tanzania Jorgen Haldorsen amesema nchi nyingine zitakazoshiriki katika majadiliano na mke wa Obama ni Peru na Cambodia.

Alisema katika kuadhimisha siku hiyo, wadau wataombwa kuunga mkono jitihada zinazofanywa na kundi hilo na kupewa nafasi ya kujifunza, kuongoza, kuamua na kuishi ili kuonesha thamani ya mtoto wa kike na hata kwa kuwapa fursa sawa.

Alisema watoto wa kike wamekuwa wakishindwa kufikia malengo yao kutokana na vikwazo kuanzia katika jamii, ambapo pindi wakiaminiwa wanaweza kufanya mambo mbalimbali katika eneo la kisiasa, kiuchumi na hata kijamii. Haldorsen alisema wasichana wa Tanzania ni miongoni mwa makundi yanayokumbana na vizuizi vingi na changamoto za kufikia maendeleo.

“Wengine hushindwa kufikia ndoto zao kutokana na kutengwa na jamii wanamoishi,” amesema.

Mkuu wa Kitengo cha Haki za Watoto na Jinsia, katika Shirika hilo Jane Mrema anasema kupitia maadhimisho hayo, Tanzania itapata fursa ya kuieleza dunia kuhusu changamoto zinazowakabili wasichana.
-BBC