Hofu ya Kimbunga Yazua Taharuki Florida, Marekani

Mkazi wa Florida akijiandaa kuhama kukimbia hofu ya kimbunga.

Mkazi wa Florida akijiandaa kuhama kukimbia hofu ya kimbunga.

 

GAVANA wa Jimbo la Florida nchini Marekani, Rick Scott ametoa tahadhari kuwa uharibifu utakaotokea utakuwa mkubwa sana ikiwa kimbunga Matthew kitapiga maeneo ya jimbo hilo.

Bw Scott ametoa wito kwa wakazi wa jimbo hilo kujiandaa kuhama makwao zoezi ambalo ndilo litakalokuwa kubwa zaidi katika historia ya jimbo hilo. Msongamano mkubwa wa magari na watu umetokea katika barabara huku watu wakihamia maeneo ya bara.

Wakazi katika jimbo la Carolina Kusini pia wametakiwa kuhama maeneo yaliyo hatarini. Gavana Nikki Haley amesema watu 250,000 watahamishwa kutoka maeneo ya pwani.

Rais wa Marekani Barack Obama amesema kimbunga hicho kinaweza kuwa hatari sana na kuwataka wakazi wa eneo hilo kufuata ushauri unaotolewa na mamlaka. Shule zimefungwa na wagonjwa wametolewa katika baadhi ya hospitali.

Kimbunga kikubwa cha mwisho kukumba jimbo la Florida kilikuwa ni Katrina miaka 10 iliyopita. Kimbunga Matthew tayari kimepiga mataifa ya Haiti na Cuba. Watu kumi wamethibitishwa kufariki nchini Haiti lakini hali halisi ya uharibifu na maafa yaliyotokea badi haijajulikana. Watu wanne wamefariki katika Jamhuri ya Dominika.