BENKI ya Posta nchini (TPB) imezindua mwezi wa uwekaji akiba duniani inayokwenda sambamba na kampeni iliyopewa jina la “Asante Mteja”.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam jana katika uzinduzi huo, Meneja wa benki ya TPB tawi la Kariakoo, Patrick Swenya alisema kuwa kampeni hiyo itaendeshwa nchi nzima katika matawi yao.
Alisema, lengo la kampeni hiyo ni kuhamasisha wateja wa TPB kuweka akiba ili kuweza kufanikisha malengo yao katika maisha ikiwemo ulipaji wa ada za wanafunzi. Meneja huyo alisema kuwa katika kuhakikisha wateja wao wanafanikiwa watatoka na kutembelea wateja wao ambao wengi ni wafanyabiashara ili kupata mrejesho wa huduma wanazozitoa ikiwemo mikopo kama imeweza kuwakomboa.
Alisema, kama watabaini mikopo inayotolewa imewanufaisha watu wengi basi watahakikisha inaboreshwa zaidi ili kuwakwamua watu wengi kiuchumi.
“Katika wiki hii ya uwekaji akiba duniani tutahakikisha sisi kama TPB tunaboresha huduma zetu ili kufanikisha zaidi Watanzania ikiwa pia ni moja ya njia ya kuwashukuru kwa kuchagua Benki yetu”, alisema Swenya. Aidha aliongeza kuwa TPB itaendelea kuboresha huduma ikiwemo mikopo ya vikundi visivyo rasmi inayotolewa kwa riba nafuu.
Kwa upande wake mmoja wa wateja wa benki hiyo Alex Lwamanya alisema kuwa mikopo ya riba nafuu inayotolewa na benki hiyo imeweza kumkwamua kiuchumi kwa kiasi kikubwa.
Alisema, hadi sasa mikopo hiyo imemuwezesha kujenga nyumba pamoja na kuendeleza biashara zake. “Nashkuru mikopo niliyoipata na ninayoendelea kupata imenikwamua kimaisha kwa kiasi kikubwa sana kwani hadi sasa nimeweza kumiliki vitega uchumi vinavyoniingizia kipato”, alisema Alex.