Na Ally Daud, MAELEZO-Dar es Salaam
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amepokea msaada wa Tsh. Milioni 60 kutoka kwa Balozi wa China nchini, Lu Youqing ikiwa ni mchango wa Serikali yao kwa ajili ya ukarabati wa shule zilizoharibika kutokana na tetemeko la ardhi lilitokea mkoani Kagera tarehe 10 Septemba, mwaka huu.
Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo leo jijini Dar es salaam, Waziri Mkuu Majaliwa aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya watu wa China kwa kuwa wameonyesha kuguswa na madhara hayo na kuahidi kuwa msaada huo utasaidia kukarabati upya miundombinu ya shule mbalimbali mkoanihumo.
“Tanzania inaishukuru kwa dhati Serikali ya Jamhuri ya watu wa China kwa kutoa msaada huu wa shilingi milioni 60 kwa kuwa utatusaidia katika kukarabati na kutengeneza shule zilizoharibika kutokana na tetemeko Mkoani Kagera” alisema Mhe. Majaliwa.
Aidha Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa aliwaomba Watanzania pamoja na makampuni mbalimbali kuendelea kuwachangia wananchi wa kagera walioathirika na tetemeko hilo ili kuwafariji na kuirudisha kagera katika hali yake ya zamani.
Kwa upande wa Balozi wa China nchini Tanzania Balozi Lu Youqing alisema wameguswa na janga hilo na kuamua kuchangia kiasi hiko cha fedha ili kuweza kukarabati shule zilizoharibika kutokana na tetemeko la ardhi mkoani humo.
Balozi Lu Youqing alisema kuwa kwa msaada huo wanaamini kwa wanafunzi wa mkoa wa Kagera ambao shule zao zimeathirika kutokana na tetemeko hilo zitasimama upya na watasoma vizuri kwenye majengo yaliyo bora na hivyo kuendelea kuinua kiwango cha elimu mkoani humo.