Na Frank Shija, MAELEZO-Dar es Salaam
WATANZANIA wameaswa kujenga utamaduni wa kulipa kodi na kudai risiti pindi wanapofanya biasha au kununua bidhaa ili kuisaidia Serikali kukusanya mapato kwa ajili ya kuendelea kutoa huduma za kijamii.
Wito huo umetolewa jana Jijini Dar es Salaam na Afisa Mwandamizi wa Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bibi. Rose Mahendeka alipokuwa akitoa elimu kwa waumini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima kuhusu umuhimu wa kulipa kodi.
Rose alisema kuwa shughuli za Serikali katika nchi yeyote duniani, ikiwemo Tanzania zinagharamiwa na fedha zinazotokana na kodi pamoja na tozo mbalimbali.
“Katika maandiko matakatifu imeandikwa; Ya Kaisari mpeni Kaisari, vya Mungu mpeni Mungu, hivyo ni vyema tukajenga utamaduni wa kulipa kodi na kudai risiti kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu”. Alisema Rose.
Alisema umuhimu wa kudai risiti kuwa ni pamoja mwananchi kutambua kiasi cha kodi anayochangia Serikali yake, kutambua kodi halisi inayotakiwa kulipwa na ushahidi wa ununuzi wa bidhaa na uhalali wa umiliki wake.
Aliongeza kuwa kutodai risiti ni kwenda kinyume na matakwa ya sheria ya mlipa kodi ambapo adhabu yake ni faini ya pointi za fedha 2 hadi 100 ambazo ni sawa na shilingi 30,000 mpaka 1,500,000/=.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Amon Mpanju aliupongeza uongozi wa Kanisa hilo kwa kuona haja ya waumini wake kupatiwa elimu ya mlipa kodi.
Aidha aliwaka waumini wa kanisa hilo kulipa kodi na kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo ya kuwa na Tanzania mpya kama ambavyo baba wa Kanisa hilo Askofu Josephat Gwajima amekuwa akisisitiza.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima Dk. Josephat Gwajima amewahimiza waumini wake kuishika na kuitumia elimu waliyopata kutoka kwa mwakilishi wa TRA ambapo aliwataka waumini hao kujenga utamaduni wa kudai risiti kila anapofanya malipo ili kusaidia ukusanyaji wa mapato ya Serikali.