Na Benedict Liwenga-WHUSM, Bukoba.
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. January Makamba amewatoa wasiwasi waathirika wa tetemeko la ardhi lilitokea Wilayani Bukoba Mkoani wa Kagera. Mhe. Makamba ameyasema hayo leo mkoani Kagera wakati wa ziara yake ya kutembelea maeneo mbalimbali yaliyokumbwa na tetemeko hilo kwa lengo la kuwapa pole waathirika na kuwap ujumbe wa Serikali kuhusu namna inavyojitahidi kuwasaidia waathirika hao.
Amesema kwamba, wananchi wasiwe na wasi wasi kuhusu suala la kupatiwa misaada ya dharura kwani Serikali imejipanga na bado inaendelea na zoezi la kufanya tathmini ya uharibifu uliotokea ingawa zoezi la kuwapatia baadhi ya huduma za msingi linaendele.
“Tumekuja kutoa msaada kwa mji kwa ujumla wakati tunapanga namna ya kusaidia katika masuala ya mazingira na tambueni kuwa Serikali inawajali ndiyo maana kuna viongozi wakubwa wako hapa na wengine wanazidi kuja”, alisema Mhe. Makamba.
Aliongeza kuwa, suala la kuwasaidia waathirika wa tetemeko hilo limepewa uzito mkubwa na Serikali na suala la kuchelewa kwa kutolewa kwa misaada kunatokana na umakini unaoendelea kufanywa sasa hivi na Serikali ili kuwatendea haki waathirika pekee.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Misenyi Luteni Kanali Denice Filangali Mwila amesema kuwa katika Wilaya yake sehemu iliyoathirika zaidi ni Kata ya Minziro ambapo jumla ya nyumba 512 haziwezi watu kuishi,pia nyumba 1,524 zenye nyufa mbalimbali zinazohitaji ukarabati, Taasisi za serikali 91 na taaisis 71 za watu binafsi ikiwemo makanisa na misikiti imeathirika na tetemeko hilo.
Ameongeza kuwa tayari amepata msaada wa Serikali katika tukio hilo kupitia Kamati ya Maafa ambapo jumla ya maturubai 520 amepewa kwa ajili ya maeneo mbalimbali, chakula, blanketi 240 ambazo pia zimegaiwa kwa waathirika hao. Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Bugandika Bw. Amudi Migeyo amewataka wananchi wake kutobeza juhudi za Serikali zinazofanywa sasa na amewataka kuridhika na chochote wakipatacho katika kipindi hiki kigumu.
Hivi karibuni siku ya tarehe 10 Septemba, 2016 mkoa wa Kagera ulikumbwa na ukubwa wa nguvu za mtetemo wa ardhi wa tetemeko la 5.7 kwa kutumia skeli ya ‘Ritcher’ ambapo jumla ya watu 17 walipoteza maisha na majeruhi kadhaa ambapo wengi wao wameshapatiwa matibabu na wanaendelea vizuri.