Na Emmanuel Shilatu Buyegu
WAKATI tunapata uhuru wetu mwaka 1961 kutoka kwa Waingereza kila Mtanganyika alikuwa na maana yake kichwani ya kuelewa nini maana ya uhuru. Wapo walioamini kuwa huo ndio utakuwa mwisho wa ubaguzi wa rangi, hadhi, kabila uliokuwa ukifanywa na Wakoloni; wengine waliamini kupata uhuru ni kufanikiwa kuziondoa tawala mbovu, nyonyaji na za kidhalimu za Wakoloni.
Licha ya mawazo mazuri waliyokuwa nayo baadhi yao, lakini kwa upande wa mwasisi mwenyewe wa uhuru wetu alikuwa na mtazamo tofauti kabisa na zilivyokuwa mawazo ya watu. Yeye Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa na maana ya kipekee kabisa juu ya dhana nzima ya uhuru.
Kwa upande wa Baba wa Taifa letu Mwalimu Nyerere aliamini na kusema ya kuwa “tumefanikiwa kuwaondoa Wakoloni na hivyo tupo huru. Na uhuru maana yake ni kazi”. Mwisho wa kunukuu.
Hapa Mwalimu Nyerere alikuwa na maana ili tuweze kupiga hatua kimaendeleo ni lazima tuutumie huu uhuru wetu vilivyo katika kupiga hatua kimaendeleo kupitia kufanya kazi kwa bidii na maarifa yetu yote ili kuleta maboresho ya kina katika Nyanja zote zile za kimaisha yaani uchumi, kijamii na kisiasa. Bila ya kufanya kazi kwa bidii, uhuru wetu ni sawa na mzoga.
Na ndio maana Mwalimu Nyerere kama kiongozi alianza kwa kuonyesha mfano wa dhahiri wa kuanzisha mapambano kwa vitendo dhidi ya maadui zetu watatu ambao ni ujinga, maradhi na umaskini.
Sehemu kubwa ya mafanikio yake yalitokana ama ni kupitia kuanzisha maazimio, mashirika, kauli mbiu na sera mbalimbali. Hayo yote aliyafanya kwa vitendo zaidi na si porojo, lawama, maandamano, wala manung’uniko.
Pia Mwalimu Nyerere alikuwa na falsafa ama dhana ya kimaendeleo ambapo aliamini maendeleo sahihi hayawezi yakapatikana nje ya uwepo wa mambo makuu manne ambayo ni “watu”, “ardhi”, “siasa safi” na “uongozi bora”.
Naam!! “Watu” ni kiungo kimoja wapo kikuu cha hakikisho la maendeleo chanya yeyote yale ndani ya familia, jamii ama Taifa kwa ujumla wake. Mathalani, endapo tutakuwa na miundombinu bora ni watu ndio wamechangia uwepo wake; ama kama tutakuwa na mazao ya kutosha kwa ajili ya chakula, biashara na kiada basi ujue ni watu wameweka jitihada za kutosha.
Halikadhalika kama kuna amani na utulivu nchini basi ujue ni watu wamechangia hilo. Jamani, hata Wahenga walisema: “usione vyaelea, ujue vimeundwa”, na waundaji wenyewe ni Wananchi (mimi, wewe na Yule).
Licha ya uwepo wa utajiri wa nguvu kazi takribani Watu Milioni 50 lakini bado watu hao hao ndani ya jamii wanachojua ni utegemezi pekee. Kivipi?
Kwa jinsi tuanavyoishi utadhani tunawangojea baadhi ya watu kutoka nje ili waje watuletee maendeleo kwetu yaani imefika kipindi kwa mtu hata kutandika kitanda chake mwenyewe anacholalia imekuwa ni kazi kubwa kwake.
Tukumbuke hivi karibuni ulitolewa utafiti uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS) uliobaini asilimia 71 ya Watanzania wanatumia muda mwingi kufanya shughuli zisizokuwa za uzalishaji mali wala tija kwa Taifa hasa za kufanya starehe mbalimbali.
Hii ni hatari sana na inaonyesha namna gani baadhi ya Watanzania tusivyojitambua. Kikubwa ambacho kinaonekana ni kujikita mizizi ya dhana nzima ya kibaguzi iliyojengeka akilini ama kwenye mitazamo ya watu ambapo tumediriki kuwaachia viongozi pekee huku tukijiengua katika kapu la dhana ya neno “serikali” wakati kiuhalisia na kimaantiki na Wananchi nao pia ni sehemu ya Serikali.
Ni kweli kabisa kwamba Serikali ni chombo cha utawala kilichoshika dola ama nchi kwa lengo la kuwaletea maendeleo Wananchi. Na wanaoiwezesha ama kuipa mamlaka hayo Serikali ni Wananchi. Bila ya watu hakuna serikali na pia Serikali haina uhalali wa kuwepo bila ya kuwepo kwa watu.
Na kundi lingine linalounda serikali ni viongozi. Hivyo serikali ni muunganiko kati ya viongozi na Wananchi. Daima na tena ni dhambi kubwa sana kuwatenganisha makundi haya (Wananchi na viongozi) katika chungu hiki Serikali.
Wananchi siku hizi wamekuwa washadidiaji wakubwa wa siasa na bila ya wao kujitambua ya kwamba hutumia muda mwingi sana kushindia na kulalia katika dimbwi la porojo za kisiasa bila ya kujibidiisha. Maendeleo yatapatikanaje bila ya sisi wenyewe kujishughulisha?
Utakuta vijana walio wengi kutwa wanashinda kwenye kucheza “pool table” na kukaa vijiweni tu; Wazee ama akina Baba nao kutwa wanacheza “bao” ama “draft” tu; na akina Mama nao kila kukicha wapo vibarazani wakisutana na kupashana umbea tu. Hayo ndio maisha ya kila siku ya baadhi ya wanajamii ya kutokupenda kufanya kazi kwa bidii.
Mwananchi huyo huyo anaitegemea Serikali ije impatie fedha mikononi bila ya yeye kujishughulisha kwa kufanya kazi yeyote ile ya kumpa kipato. Hakuna Serikali yeyote ile duniani inayoweza kuwapatia wananchi wake pesa lukuki bila ya wao kujishughulisha.
Kama hauamini, jaribu kufanya utafiti katika nchi zilizoendelea utakubaliana nami kuwa hakuna Taifa lolote lile lenye raia wasiojibidiisha kwa kutegemea mteremko kutoka kwa Serikali zao. Yatazame mataifa kama ya Marekani, Uingereza, China au Urusi wakazi wake wanavyotambua ya kuwa thamani ya pesa yao na uchumi wa nchi unategemea zaidi ni kwa jinsi gani watu wa ndani (wao wenyewe) wanavyozalisha mali.
Lakini sie hatujitambui na tupo bize kwa kujiteketeza na porojo kila uchwao. Hapa tumesaliti Mwalimu Nyerere na alivyoamini maana ya uhuru kuwa ni kufanya kazi kwa bidii, umasikini hautatuacha kweli? Nani wa kulaumiwa ni serikali na viongozi wake ama ni sisi Wananchi?
Hii yote inatokana na jamii kuziasi mitazamo miongozo na falsafa za Mwalimu Nyerere (mathalani ile ya “Uhuru ni kazi”) hali inayosababisha kiwango cha idadi ya watu maskini kuzidi kukua nchini licha ya kujaariwa rasilimali na mali za asili kwa kuyachakachua maendeleo yetu wenyewe. Kisa? Porojo kutawala maisha yetu.
Tusiishie kuwalaumu tu Viongozi wetu kila kukicha huku tukisahau jinsi sisi tulivyo wavivu sana wa kupindukia. Watanzania tulio wengi hatupendi kufanya kazi kwa bidii na kwa ubunifu. Watanzania tulio wengi hatupendi njia nyoofu na sahihi badala yake tunapenda njia ya mkato ya kujipatia vipato vyetu. Watanzania wengi tunapenda sana kufanya madili, ama “michongo” kama wanavyoita watoto wa mjini.
Kwenye salam zao ama maongezi mengi ya Watanzania ni nadra sana kukosa kusikia maneno kama vile “mambo mengine niaje, ishu vipi ama madili yakoje”. Ni dhahiri kuwa hapa inatafutwa njia ya mkato ya mafanikio katika maisha. Hali hii huzaa matokeo endelevu mabovu ndani ya jamii kama vile utapeli; ujambazi; ongezeko la mihadarati na madawa ya kulevya; mauaji ya maalbino na vikongwe; pamoja na uchafu ama uozo mwingine kadha wa kadha unaofanana na huo.
Chanzo haswa cha uwepo wa utafutaji mambo kwa njia ya mkato halijasababishwa na Viongozi ndani ya Serikali bali msingi wake mkuu ni Watu tulio wengi kutaka matokeo chanya yenye faida na matunda kwa haraka na hata pia kukata tama ya kimaisha kwa haraka zaidi kutokana na kujinyima fursa ya uvumilivu na ustahimilifu ndani yetu.
Mapambano ya maisha ni sawa na vita kali ambapo si tu jukumu la viongozi bali hata nasi Wananchi tuna wajibu mkubwa wa kufanya kazi kwa bidii na si kulalama tu kila kukicha.
Kuna usemi mmoja unaosema “Wanaofanikiwa zaidi ni wale walioshindwa mara nyingi” Je utashindwaje, kama hujajaribu mara nyingi? Je mafanikio katika maisha yanapatikana kwa mara moja tu? Haya ni maswali muhimu na ya msingi sana kwa Watanzania, kujiuliza.
Ifike mahali tujitambue ya kwamba kelele, tuhuma, lawama, dharau kwa viongozi wetu hazitatusaidia endapo sisi kwa sisi hatujaamua kujibidisha ipasavyo. Utakuta ndani ya jamii fulani tupo zaidi ya watu laki mbili lakini tunamtegemea kiongozi mmoja tu awe ni Mbunge ama Diwani ili aweze kutuletea maendeleo. Endapo sisi tulio wengi tumeshindwa kuwa kitu kimoja wenye nia moja ya umoja, mshikamano na tukaamua kwa dhati kujiletea maendeleo; Je, kiongozi mmoja pekee atawezaje?
Ndugu zangu, kwanini alaumiwe dobi kutakasa kaniki wakati tunajua rangi ya kaniki? Ni lazima tutambue ya kwamba sisi raia pia tunahusika vilivyo na huu umaskini wetu na si vyema kuwasukumizia mzigo wote wa lawama viongozi wetu pekee. Watanzania tulio wengi tunapoteza muda mwingi kwa kukaa vijiweni, kushabikia siasa tu, kupiga soga na kucheza bao muda wote. Je, tukiamua kujishughulisha kwa kuutumia muda huo ipasavyo tungekuwa wapi kimaendeleo hivi sasa?
Waswahili walisema usimuhadithie mtu ndoto yako uliyoota jana usiku lakini hapa ni kinyume kwani siri tunasema na bayana tunaambizana. Binafsi huwa Napata ukakasi pindi nionapo Serikali ina sera na majukumu lukuki lakini Watanzania tulio wengi hatushiriki vyema na hata hatutimizi wajibu wetu kwa wakati. Mwenye jukumu la kulifuatilia Taifa letu kwa ukaribu na utendaji ni serikali pekee ama na Wananchi pia? Je, kwa uwajibikaji huu, maisha bora kwa kila Mtanzania yatapatikana kweli?
Mara nyingi sera tulizonazo zinategemea zaidi umoja, mshikamano, ushirikiano na nia ya dhati ya uwajibikaji wa pamoja kiutekelezwaji. Kamwe maisha bora kwa kila Mtanzania hayaji kwa kuota au kupiga soga ama kwa kungojea mpaka uone Tanzania (nchi yako) imekufanyia nini na badala yake ujiulize wewe mwenyewe umeifanyia nini Tanzania?
Kuna wanamapinduzi, wanaharakati na watu mashuhuri wengi tu hapa Duniani ambao hawakungoja mpaka waone nchi zao zimewafanyia nini na badala yake walijiuliza wamezifanyia nini nchi zao?
Mwalimu Julius Nyerere, Nelson Mandela, Martin Luther King Jnr, Kwame Nkurumah, Chifu Mkwawa ni baadhi tu ya Wanaharakati na wakombozi wa kweli dhidi ya Uhuru na ubaguzi wa ngozi nyeusi ambao milele na milele watabakia kuwa ni mashujaa maarufu wa ulimwengu. Jiulize mwenyewe wewe je utakumbukwa, ama tutajivunia nini kutoka kwako? Je, ni kwa huo ugoigoi wako ama kwa uwajibikaji wako?
Tuache uvivu na tujitume vilivyo kwa kuchangamkia fursa na Baraka tulizojaaliwa. Mungu ametujaalia wingi wa ardhi yenye rutuba ifaayo kwa kilimo, misitu, wanyama pori na vyanzo vingi vya kujiletea maendeleo.
Hata kama Rais John Pombe Magufuli ni mzuri kiasi gani hatoweza kuleta maendeleo tarajiwa kwa Watu endapo sisi wenyewe Watanzania (Watu) hatutafanya kazi kwa bidii na badala yake tutasikia uchumi wa Taifa umekuwa lakini pato binafsi la Mtanzania likiendelea kushuka. Dawa ya kukuza mapato binafsi ni kwa kufanya kazi kwa bidii kwa kuzichangamkia fursa za kiuchumi tulizojaaliwa.
Tanzania isiyo na maradhi inawezekana; Tanzania yenye uchumi imara mpaka kwa Wananchi wake inawezekana; Tanzania yenye huduma bora zaidi za kijamii inawezekana; Hakika Tanzania yenye maisha bora zaidi pia inawezekana. Hii itawezekana tu endapo kila mmoja wetu atatimiza wajibu ipasavyo kwake na kwa Taifa lake.