Na Beatrice Lyimo, Maelezo – Dar es Salaam
WAKALA ya Mkemia Mkuu wa Serikali imekusudia kuendesha kampeni maalum ya kupima matumizi ya vilevi kwa madereva wanaosafirisha abiria na mizigo ikiwa ni hatua ya kukabiliana na tatizo la ajali za barabarani nchini.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkemia Mkuu wa Serikali Prof. Samwel Manyele alipokuwa akifungua mafunzo ya siku mbili kwa wadau wa kemikali juu ya matumizi salama ya kemikali nchini.
Prof. Manyele alisema utaratibu wa kuwapima madereva hao utaanza hivi karibuni na utawezesha kupunguza tatizo la ajali barabarani na kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama kutoa ushirikiano katika zoezi hilo.
“Madereva wote wanaosafirisha mizigo na abiria watatakiwa kupita kwenye kipimo ambacho kitaonyesha kama madereva hao wanatumia vilevi, hali hiyo itasaidia kutatua tatizo la ajali za barabarani nchini,” amesema Prof. Manyele.
Aidha, Prof Manyele alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kutoa uwezo na uelewa kwa wahusika hasa wasimamizi wa shughuli za kemikali na matumizi salama juu ya kukabiliana na matukio au ajali za kemikali pale yanapotokea.
Aliongeza kuwa mafunzo hayo yamekuja kufuatia uelewa mdogo wa elimu kwa baadhi ya wadau wanaojishughulisha na masuala ya kemikali kuhusu uzalishaji, uhifadhi, usimamizi na usafirishaji wa matumizi ya kemikali nchini.
Mbali na hayo, Prof Manyele alisema kumekuwa na ajali na matukio yanayotokana na kemikali ikiwemo ya ajali halisi na mengine kutokana na kukosa uelewa wa matumizi sahihi na salama ya kemikali.
Akifafanua zaidi Prof. Manyele alisema katika kukabiliana na madhara yatokanayo na matumizi yasiyo salama ya kemikali, Serikali ilitunga sheria ya Kemikali za Viwandani na majumbani mwaka 2003 kwa lengo la kuhakikisha kemikali hizo zinatumika katika hali iliyo salama.