KAMATI ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imekifungulia Kituo cha Radio cha Magic FM na kukipa masharti, huku ikiendelea kukifungia kituo cha Radio 5 cha jijini Arusha. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui, Joseph Mapunda Magic FM imefunguliwa kuanzia kesho na inatakiwa kumuomba radhi Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, wasikilizaji na wananchi kwa ujumla.
Alisema tangazo la kuoimba radhi litolewe kwa siku tatu mfululizo katika taarifa za habari za saa kumi jioni na saa tatu usiku kuanzia tarehe 17/09/2016 hadi tarehe 19/9/2016 na tangazo la kuomba radhi lipewe nafasi kubwa katika kipindi cha taarifa ya habari hizo, huku wakipewa onyo kali.
Alisema baada ya kusikiliza na kutafakari kwa kina maelezo ya utetezi yaliotolewa na uongozi wa Magic FM Radio imeridhika kuwa kipindi cha Morning Magic kilikiuka baadhi ya kanuni za huduma za utangazaji za mwaka 2005. Alizitaja kanuni zilizokiukwa ni pamoja na 5(a),(b), (c), (d), (f), (h), 6(2) (b) (c) na 18 (i) (b) (i) (ii) (iii) hivyo kupewa adhabu iliyotajwa hapo juu.
Akitoa hukumu ya kituo cha Radio 5, Makamu Mwenyekiti huyo alisema baada ya kusikiliza na kutafakari kwa kina maelezo ya utetezi yaliyotolewa na uongozi wa kituo hicho cha jijini Arusha, alisema kamati yake imeridhika kuwa kipindi cha Matukio cha radio hiyo kilikiuka baadhi ya kanuni za Huduma za Utangazaji (Maudhui) 2005 na kimetozwa faini ya shilingi milioni 5 ambazo zinatakiwa kulipwa ndani ya siku 30 kuanzia iliposomwa hukumu (16/9/2016).
Kanuni zilizokiukwa ni pamoja na 5(a), (b), (c), (d), (f), (h), 6(2) (b) (c) na 18(1) (b) (i), (ii) (iii), ambapo tarehe 25/8/2016 Radio 5 kupitia kipindi chake cha Matukio kilichorushwa hewani kati ya saa 2.00 usiku na saa 3.00 usiku, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alitamka maneno ya kashfa yaliolenga kumdhalilisha Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli na Serikali yake pamoja na kuhamasisha wananchi kuvunja sheria halali.
Alisema adhabu nyingine kwa Radio 5 ni pamoja na kufungiwa kwa miezi mitatu kuanzia 16/9/2016 na itakapofunguliwa itawekwa chini ya uangalizi maalumu kwa muda wa mwaka mmoja. Hata hivyo alisema vituo vyote vina haki ya kukata rufaa ndani ya siku 30 tangu kusomwa kwa hukumu yao endapo vitaona havijaridhishwa na hukumu hiyo.
Awali katika maelezo ya hukumu uongozi wa Radio 5 uliomba radhi kwa muonekano wowote au makosa katika kipindi kilichorushwa siku ya tarehe 25 Agosti, 2016 na kuomba kamati izingatie kuwa kituo hicho hakijawahi kuvunja kanuni zozote za utangazaji tangu kufunguliwa kwake, pia kuzingatia ushirikiano walioutoa kwenye maelekezo ya mamlaka na izingatie mikataba ya matangazo na ajira za wafanyakazi takribani 30 wa kituo hicho.