Na Mwandishi Wetu
JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limetangaza tarehe ya kuanza kwa maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani ambapo mwaka huu inatarajia kufanyika kitaifa Mkoani Geita. Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, DCP Mohamed Mpinga alisema maadhimisho ya mwaka huu yamepewa kauli mbiu ya ‘Hatutaki Ajali – Tunataka Kuishi Salama’ hivyo kuwataka madereva na watumiaji wengine wa usalama barabarani kuhakikisha suala la usalama barabarani linaimarika.
Kamanda Mpinga alisema ongezeko la vyombo vya moto barabarani, kwa upande mmoja na ule wa ongezeko la watumia barabara wa ngazi na aina mbalimbali kwa upande mwingine, hauna budi kutiliwa maanani hasa linapozungumziwa suala la ajali za barabarani.
Alisema bado ubovu na uharibifu wa vyombo vya moto vinavyotembea barabarani ni miongoni mwa sababu kuu tatu zinazosababisha ajali na kutufikisha katika hali ya kuathiri hali ya usalama katika barabara zetu. Alisema kauli mbiu ya mwaka huu inasisitiza kila mtumiaji wa barabara kuwa anawajibu wa kuhakikisha usalama barabarani unaimalika.
“Ni dhahiri kwamba suala la usalama barabarani siyo la kundi au taasisi moja tu, ila ni letu sote. Wanahabari ni miongoni mwa wahusika wa suala la usalams barabarani, kwa maana mnayo nafasi kubwa ya kuuelimisha umma na kusaidia katika suala la ujenzi wa utamaduni wa usalama barabarani nchini,” alisema Kamanda Mpinga.
Alisema miongoni mwa shughuli ambazo zitafanyika katika maadhimisho ya mwaka huu ni pamoja na kutoa elimu kwa watumiaji barabara wote, kufanya ukaguzi wa vyombo vya moto kama magari, pikipiki na bajaji; ikiwemo kuwataka watumiaji kuzingatia sheria, kanuni na utaratibu wa usalama barabarani.
Aliongeza kuwa zoezi la ukaguzi litafanyika pamoja na utoaji wa stika maalum za usalama barabarani kwa vyombo ambavyo vitathibitika kuwa na ubora wa kutembea barabarani, hivyo kuwataka wananchi wenye vyombo vya moto kuvipeleka katika vituo vya polisi kitengo cha ukaguzi kwa ajili ya kukaguliwa.
Aidha alisema gharama za ukaguzi kwa mwaka huu itakuwa ni shilingi 5,000 kwa magari ya biashara, shilingi 3,000 kwa magari madogo ya binafsi na shilingi 1,000 kwa pikipiki na bajaji. Aliwataka wamiliki kupeleka vyombo hivyo katika vituo vya ukaguzi vya kikosi cha usalama barabarani kwa ajili ya magari yao kukaguliwa.