BENKI ya Posta Tanzania (TPB) imetoa msaada wa madawati 43 yenye thamani ya Milioni 3.5 kwa Shule ya msingi Mbande iliyopo kata ya Chamanzi Wilaya ya Temeke.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya madawati hayo mwishoni mwa wiki Ofisa Mawasiliano wa TPB Chichi Banda, alisema shule hiyo ilituma maombi kwao kwa ajili ya kutatuliwa changamoto ya madawati nao waliguswa ndio maana wameona ni vema kutoa msaada huo.
Alisema madawati hayo yatawasaidia wanafunzi kusoma vizuri pasipo kupata adha yoyote pale wanapokuwa wakimsikiliza Mwalimu pamoja na kuwapuguzia adha ya kukaa chini. Banda alisema benki hiyo imekuwa ikitoa kipaumbele katika sekta ya elimu kutokana na ukweli usiopingika kuwa elimu ni uti wa mgongo wa taifa lolote hapa duniani.
“Msaada huu tuliotoa leo ni sehemu ya benki yetu pamoja na kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano ya kumaliza tatizo la uhaba wa madawati katika shule za msingi” alisema Banda. Banda alisema benki hiyo imekuwa ikifanya kazi kwa ukaribu na wananchi na kuwa sehemu ya kwanza kuikimbilia ili kutatua changamoto mbalimbali katika mazingira yanayowazunguka. Aidha alitoa wito kwa wanafunzi wa shule hiyo kusoma kwa bidii pamoja na walimu kuongeza juhudi katika kuwafundisha ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Mashaka Mwakyambiki, aliishukuru benki hiyo kwa kutoa mchango wa madawati ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora katika mazingira mazuri na rafiki. Alisema hapo awali wanafunzi walikuwa wakisoma wakiwa wamekaa nchini jambo ambalo lilikuwa likisababisha kutokufanya vizuri darasani. “Tunaishukuru sana TPB kwa kuguswa na ombi letu la upungufu wa madawati na kuamua kutusaidia iliwanafunzi wetu waweze kusoma katika mazingira mazuri” alisema Mwakyambiki. Mwakyambiki alisema shule hiyo bado ina uhaba wa Madarasa ya kusomea pamoja na uzio na kuomba wadau kujitokeza na kuiga mfano wa TPB.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya shule hiyo George Anania, kwa niaba ya wazazi alisema TPB imeonyesha ukomavu wa hali ya juu kwa kujitokeza na kutoa msaada wa madawati hayo jambo ambalo ni kuigwa. “Mfano huu ni wa kuigwa na wadau wengine kujitokeza kusaidia madawati kutokana na kuwa ni changamoto kubwa ambayo imekuwa ikisababisha wanafunzi kushindwa kufanya vizuri” alisema Anania
Naye mwanafunzi kutoka shule hiyo Ashura Ibrahim alisema hapo awali walikuwa wakichafuka sare zao kutokana na kusoma wakiwa wamekaa chini kupitia madawati hayo watasoma kwa juhudi na bidii zaidi.