Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Usalama na Mazingira (Mazingira), wa Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Melania Sangeu amezungumzia umuhimu wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS),kushirikiana na Halmashauri za wilaya katika kuhifadhi machimbo ya mawe na mchanga yaliyotumiwa kwa shughuli za ujenzi wa barabara ili kulinda mazingira na kuepusha ajali.
Eng. Sangeu amesema hayo mjini Katesh wilayani Hanang alipokuwa akikagua usalama wa mazingira katika maeneo yaliopitiwa na barabara za lami mkoani Manyara.
“Hakikisheni mnawabana makandarasi kabla ya kuondoka katika maeneo ya miradi ya barabara wawe wamehifadhi maeneo waliyotumia kuchimba mawe na mchanga kama wanavyoelekezwa na na tathmini ya athari kwa mazingira (environment impact assessment)”. Amesema Eng. Sangeu.
Amewataka TANROADS kushirikiana na halmashauri ili maeneo yanayotumiwa kuchimba mawe na mchanga yahifadhiwe ili yasivamiwe na wananchi hali inayoweza kuleta uharibifu mkubwa wa mazingira na miundombinu iliyokusudiwa.
Eng. Sangeu yuko mkoani Manyara katika ziara ya kukagua usalama wa mazingira katika miradi ya ujenzi wa barabara zilizokamilika kwa kiwango cha lami ambapo amekagua ujenzi wa barabara ya Katesh- Dareda Km 67, Dareda-Babati-Minjingu Km 84 na Babati-Bonga KM 16.
Zaidi ya barabara zenye urefu wa KM 1446 mkoani Manyara bado hazijajengwa kwa kiwango cha lami katika wilaya za Kiteto, Mbulu, Simanjiro, Hanang na Babati hivyo elimu kwa wananchi ikitolewa mapema itasaidia kulinda usalama wa mazingira pindi ujenzi wa barabara hizo utakapoanza.