Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Simu Tanzania (TTCL) imesema inamajibu ya mawasiliano ya uhakika kwa wahandisi wanaofanya kazi zao maeneo yasio na mawasiliano na sasa imeanza kutoa huduma hiyo kwa wahandisi hao ili waweze kutekeleza kazi zao kwa ufanisi.
Kauli hiyo imetolewa na Mhandisi Mratibu wa Huduma Mpya za TTCL, Yonah Kulanga akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa 14 wa Wahandisi jijini Dar es Salaam ambapo kampuni hiyo imewahakikishia wakandalasi hao kuwa ipo tayari kusaidia kutoa mawasiliano hata maeneo yasio na mifumo ya kawaida ya mawasiliano nchini.
Alisema mawasiliano ni miongoni mwa nyenzo muhimu kwa makampuni hayo hivyo TTCL inamajibu ya kutoa mawasiliano hata kwa maeneo ambayo hayana mfumo wa mawasiliano wa kawaida kwa kufunga vifaa maalumu ambavyo vinasaidia kampuni hizo kufanya mawasiliano yao wakiwa kwenye maeneo ya kazi. Alisema wahandisi wanafanya tafiti na mawasiliano nje na ndani ya nchi hivyo kuhitaji mawasiliano ya uhakika wakati wote wawapo kazini.
Aliongeza kuwa wakandarasi wamekuwa wakifanya kazi maeneo ya porini sehemu ambazo hazina mawasiliano ya mkongo, wala kopa na hata mawasiliano ya redio jambo ambalo TTCL imeleta mapinduzi kwa wakandarasi hao ili kuweza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na bila vikwazo vya mawasiliano. “…Kwa maeneo kama haya ambayo hayana mawasiliano TTCL tumekuja na majibu kwa wahandisi katika maeneo kama haya tunaweza kuwapatia wahandisi mawasiliano ya intaneti kwa kutumia mawasiliano ya sateliti, yaani tunafunga vifaa maalumu vinavyo saidia kupata mawasiliano eneo husika…,” alisema Kulanga.
Alisema kwa sasa maeneo yote ya Tanzania TTCL inaweza kutoa huduma hizo kwa wahandisi watakao hitaji
Aidha alisema huduma hii imesha tolewa, yataja maeneo ambayo wamesha toa huduma hizo kuwa ni pamoja na Rukwa kwa baadhi ya mbuga, Lindi Londo Forest, Mbuga ya Serengeti maeneo ya utafiti, Kituo cha Tawiri, Kituo cha Utafiti Makutupora Dodoma, Maeneo ya Ufugaji Kongwa, mbayo hayana mawasiliano kama wakanda.
Kwa upande wake, Mhandisi wa Mkongo wa Taifa, Nsaji Mwamukonda alisema wahandisi wanapewa fursa kubwa ya kutumia mkongo pamoja na faida zake kwenye shughuli zao hivyo kuwataka pia kutumia kituo mahiri cha kutunzia taarifa (Data Centre) kinachoendeshwa na TTCL katika kuhifadhi taarifa zao kwa usalama.
Alisema wahandisi wana taarifa muhimu ambavyo hutumika kwa shughuli mbalimbali hivyo hazina budi kuhifadhiwa sehemu salama na ya uhakika hivyo kuwaomba wajitokeze kukitumia kituo hicho cha kuhifadhi taarifa. “…Wahandisi wetu wanataarifa muhimu katika kazi zao na nyingine wamekuwa wakizitegemea kwenye tafiti hivyo nashauri makampuni haya kukitumia kituo chetu kuhifadhi taarifa zao kiusalama,” alisema Mwamukonda.
Mkutano Mkuu wa 14 wa Wahandisi unafanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam Septemba 1 na 2, 2016 katika viwanja vya Mlimani City ambapo makampuni na taasisi mbalimbali wadau wa wahandisi ikiwemo TTCL zimeshiriki kufanya maonesho juu ya huduma na bidhaa anuai kwa wajumbe kwenye mkutano huo.