MAANDALIZI ya maadhimisho ya wiki ya unywaji wa maziwa Shuleni, ambayo hufanyika Septemba 28 kila mwaka duniani yamepamba moto mkoani Arusha ambapo maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika kitaifa mjini hapa.
Kanda ya Kaskazini ambao ni wenyeji wa maadhimisho hayo ya kitaifa,yatahudhuriwa na wadau wa uzalishaji maziwa viwandani wakiwemo baadhi ya wafanyabiashara wa bidhaa hiyo pamoja na viongozi wa kitaifa.
Mwenyekiti wa maandalizi ya maadhimisho hayo Peter Ngasa ambaye ni Mkurugenzi wa Kiwanda cha Maziwa cha Arusha Diary, alisema kuwa tayari wamewaalika wadau mbalimbali.
Ngasa alisema kuwa wanafunzi kutoka shule nne za Msingi Mkoa wa Arusha na wanafunzi kutoka shule sita za Mkoa wa Kilimanjaro wameaalikwa katika maadhimisho hayo na kuwa maziwa yatatolewa bure kwa wanafunzi na wadau watakaohudhuria maadhimisho hayo.
Alisema kuwa wadau wa maziwa wameandaa tisheti, kalamu na vivutio vingine kwa ajili ya wanafunzi watakaoshiriki katika maadhimisho hayo. Aliwataka wadau wote wakiwemo walezi kuhimiza watoto kushiriki sherehe hizo ili waweze kujifunza na kujua umuhimu wa maziwa katika makuzi yao.
Alifafanua kuwa kabla ya kuanza maadhimisho hayo yataanza maandamano yatakayoanza katika ofisi za Mkuu wa Mkoa kupitia Polisi na baadaye katika viwanja vya shule ya msingi Kaloleni.