Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angela Kairuki amewasisitiza watumishi wa Umma kufahamu kanuni za kudumu za utumishi wa umma ili kutambua haki zao na kuepuka kunyanyaswa na waajiri wao.
Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri huyo alipokuwa akiongea na mwandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa mipango na mikakati iliyowekwa na wizara yake katika kipindi cha uongozi wa awamu ya tano.
Waziri Kairuki amesema kuwa ni muhimu kwa watumishi wa Umma kufahamu kwa undani maadili yaliyowekwa na Serikali kwa ajili yao kwa kuwa yatawasaidia kufanya kazi kwa uadilifu wa hali ya juu.
“Inawezekana maafisa utumishi walikuwa wakizishikilia kanuni za utumishi wa umma na kuona kama ni za kwao kana kwamba mtu mwingine hatakiwi kuzifahamu lakini napenda kutoa rai kwa watumishi wote kuwa kanuni hizi ni za kwetu wote hivyo ni muhimu kuzifahamu”, alisema Mhe. Kairuki.
Mhe. Kairuki ameongeza kuwa kanuni za utumishi za mwaka 1994 zilirekebishwa na kwa sasa kanuni zinazotumika ni za mwaka 2009 ambazo zinapatikana katika tovuti za wizara mbalimbali hivyo upatikanaji wake umerahisishwa tofauti na zamani.
Pia amewataka watumishi kufuatilia waraka mbalimbali wa maendeleo ya kiutumishi inayotolewa na wizara hiyo kwa kuwa itawasaidia kufahamu miundo mipya ya utumishi inayotolewa, endapo mtumishi hatofahamu mabadiliko hayo atakosa taarifa muhimu.
Aidha, Waziri huyo amewakumbusha Maafisa Utumishi kuwa kazi hiyo wamesomea na watumishi ndiyo wadau wao wakubwa hivyo kwa namna moja ama nyingine kazi yao kubwa ni kuwasimamia na kuwahudumia vyema watumishi hao katika maeneo yao ya kazi.
“Napenda kutoa agizo kwa Maafisa Utumishi wote kufanya kazi zenu kwa umakini kulingana na kanuni za utumishi, kwa kuwa kazi hiyo mmeisomea basi ni lazima muwahudumie vizuri watumishi ili nao waweze kupata ufanisi zaidi wa kutekeleza majukumu yao”, alimalizia Mhe. Kairuki.