NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani (Mb) amewataka wataalamu wa Teknolojia ya habari na Mawasiliano nchini kufanyakazi kwa weledi na uzalendo katika nchi yao ili taaluma hiyo isaidie kukuza uchumi na kufikiwa kwa uchumi wa Viwanda vya gesi asilia, viwanda vya kati na viwanda vya usindikaji wa mazao.
Ngonyani aliyasema hayo wakati akifungua warsha ya wataalamu wa teknolojia ya habari na mawasiliano katika ukumbi wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es salaam.
“Fanyeni kazi kwa weledi bidii na uzalendo ili taaluma hii isaidie katika kukuza uchumi katika sekta ya viwanda hapa nchini alisema, Waziri Ngonyani.
Pia alieleza kuwa teknolojia ya Habari na Mawasiliano inaweza kutumika kwenye uchukuzi, kukuza sayansi na teknolojia, kukuza biashara na kuongeza uzalishaji katika kilimo na itawasaidia wananchi kujiajiri.na kuajiriwa.
Aidha alisema kuwa Tanzania imejiwekea malengo ya maendeleo ya muda mrefu na katika utekelezaji wa dira hii umegawanywa kwa vipindi vya miaka mitano mitano ambapo kipindi cha kwanza kilikuwa mwaka 2011/2012 – 2015/2016 hadi kufikia 2025.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia sekta ya mawasiliano Profesa Faustin Kamuzora amesema Serikali ilifanya uchunguzi kuhusu changamoto na mafanikio kwenye utambuzi wa TEHAMA kwenye sera ya mwaka 2003.
Katika uchunguzi huo upande wa changamoto ilibaini kuwa Tanzania haikuwa na bodi rasmi ya kusimamia, kutambua, kutathmini na kukuza wataalamu waliobobea katika teknolojia ya habari na Mawasasiliano yaani TEHAMA, ila kwa sasa changamoto nyingi zimeshagundulika na kufanyiwa kazi katika sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2016 ambayo ilizinduliwa tarehe 16 Mei, 2016 mjini Dodoma.
Tanzania inatambua umuhimu wa Tehama katika kuwezesha sekta nyingine katika harakati za kuleta maendeleo na kwa sasa kuna ongezeko kubwa la vijana wenye taaluma hiyo kwa kuwa kuna vyuo mbalimbali ambavyo zinatoa mafunzo kwa vijana katika fani ya teknolojia ya habari na mawasiliano na matumizi ya kompyuta.
Alisema kuwa kuundwa kwa TEHAMA ni nguvu za serikali kwa madhumuni ya kukuza taaluma na maendeleo kwenye teknolojia hiyo ili kusaidia serikali kufanya maamuzi kwa kuzingatia matokeo ya uchunguzi wa kisayansi. Alimalizia kwa kusema kuwa ile ndoto ya muda mrefu ya kuwa na bodi ya wataalamu wa teknolojiaya habari na mawasiliano sasa imekuwa halisia.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA Mhandisi Samson Mwella alisema ongezeko la asilimia 10 ya eneo ambalo halijafikiwa na matumizi ya Tehama kufikisha huduma kwa wananchi kwa kawaida kumechangia asilimia 1.38 kwenye pato ghafi la Taifa..