Rais Magufuli Apokea Taarifa Maendeleo ya Ujenzi wa Kiwanda cha LNG

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli leo tarehe 22 Agosti, 2016 amepokea taarifa ya maendeleo ya mradi mkubwa wa ujenzi wa kiwanda cha kusindika gesi asili (LNG Plant) kinachotarajiwa kujengwa katika eneo la Likon’go, Mchinga Mkoani Lindi.

Mwakilishi Mkazi wa Kampuni ya Statoil ya Nchini Norway ambayo ni moja ya Kampuni zitakazowekeza katika mradi huo Bw. Oystein Michelsen amemueleza Rais Magufuli kuwa ujenzi wa kiwanda hicho unatarajiwa kugharimu Dola za Kimarekani Bilioni 30 sawa na zaidi ya Shilingi Trilion 65 za Kitanzania na kwamba uzalishaji unatarajiwa kuchukua muda wa zaidi ya miaka 40 baada ya kuanza.

Bw. Oystein Michelsen amebainisha kuwa Serikali ya Norway ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa manufaa ya pande zote na ameomba Serikali ya Tanzania iendelee kutoa ushirikiano ili kufanikisha ujenzi wa kiwanda hicho.

Kwa upande wake Rais Magufuli amemuhakikishia Mwakilishi huyo wa kampuni ya Statoil kuwa Serikali ya Tanzania ipo tayari kuhakikisha mradi unafanikiwa na ameitaka Wizara ya Nishati na Madini kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) kushirikiana na wadau kutoka Wizara nyingine kuharakisha mchakato wa kuanza kwa ujenzi wa kiwanda hicho.

“Nataka kuona mradi huu unaanza kujengwa, tunachukua muda mrefu mno, kamilisheni mambo yaliyobaki ili wawekezaji waanze kazi mara moja” Amesema Rais Magufuli.

Dk. Magufuli amesema mradi huo unatarajiwa kuzalisha ajira kwa idadi kubwa ya watanzania na utaiwezesha serikali kupata mapato kupitia tozo mbalimbali, na hivyo kutumika kuimaisha huduma za kijamii zikiwemo elimu, afya, maji na miundombinu.

Pamoja na Statoil kampuni nyingine zinazoshiriki katika uwekezaji wa mradi huu ni Shell, Exxon Mobil, Pavillion na Ophir.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es Salaam
22 Agosti, 2016