Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), leo saa 6:00 usiku litafunga tena dirisha la usajili baada ya kulifungua jana kwa saa 48 na imebainika kuwa timu tatu zaidi zilikuwa na dosari katika usajili hivyo kufanya ongezeko la kutoka timu nane zilionekana kwa haraka mapema wiki hii mara baada ya dirisha kufungwa Agosti 6, 2016.
Timu hizo kwa ujumla zilikuwa na dosari ya ama kutokusajili kabisa au kutokamilisha usajili wa ushiriki wa ndani kwa msimu wa 2016/2-17.
Timu tatu nyingine zilizobainika leo Agosti 14, 2016 katika mtandao ni pamoja na Toto African ya Mwanza na Stand United ya Ligi Kuu Tanzania Bara kadhalika Arusha FC ya Arusha ambayo msimu huu itashiriki Ligi Daraja la Pili (SDL).
Hadi tunatuma taarifa hii usajili ulikuwa ukiendelea kwa mfumo wa mtandao (TMS) ikiwa na maana ya Transfer Matching System, lakini Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limerejea kanuni za usajili hivyo kuzitoza faini timu zilizokuwa na dosari. Faini imetozwa kwa viwango tofauti kulingana na mashindano.
Timu zinazohusika na usajili wa mtandao ni zile zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Ligi Daraja la Kwanza la StarTimes (SFDL) na Ligi Daraja la Pili (SDL) na adhabu ya kushuka daraja na kwenda kushiriki Ligi ya Wilaya kisha Ligi ya Mabingwa Mikoa (RCL) ambayo usajili wake ni wa kutumia karatasi.
Timu za Ligi Kuu ambazo zilikatiwa mawasiliano baada ya kushindwa kuwahi tarehe ya mwisho ya usajili ni Young Africans ambayo haikusajili kabisa. Kwa kufanya makosa hayo, kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu ya Vodacom, Young Africans imeadhibiwa faini ya shilingi milioni tatu (Sh. 3,000,0000). Young Africans imetozwa faini hiyo kwa kutosajili jina hata moja kabla ya Agosti 6, 2016.
Timu nyingine za Ligi Kuu ambazo hazikukamilisha usajili angalau kufikisha wachezaji 18 ni African Lyon ya Dar es Salaam, Stand United ya Shinyanga na Toto African ya Mwanza ambazo kila timu imetozwa faini ya shilingi milioni moja (Sh.1,000,000).
Kwa timu za Daraja la Kwanza la StarTimes (SFDL), Coastal Union ya Tanga pekee imetozwa faini ya shilingi milioni moja (Sh.1,000,000) wakati timu nyingine za daraja hilo, Kiluvya United na Friends Rangers za Dar es Salaam pamoja nna Panone, zimetoswa faini ya shilingi laki tano (Sh. 500,000) kila moja.
Kadhalika kwa timu za Daraja la Pili (SDL), ambazo ni Kitayose ya Kilimanjaro, Mashujaa ya Kigoma na Arusha FC ya Arusha, zimetozwa faini ya shilingi laki tano (Sh. 300,000) kila moja. Faini hiyo ni kwa timu na uongozi husika hauna budi kuilipa mara moja, kwani TFF haitatoa leseni za wachezaji kama timu haijalipwa faini hiyo.
Kanuni zinazozungumzia usajili ni Sura ya 10 inayozungumzia usajili na 11 inayozungumzia Adhabu Zihusuzo Usajili Na Uhamisho kadhalika Uhamisho Nje ya Nchi.