Na Mwandishi Wetu,
KAMPUNI ya Simu Tanzania (TTCL) imesema ipo tayari kutoa huduma za Mawasiliano za kisasa kwa Taasisi za Umma zinazohamia mkoani Dodoma kama ambavyo imekuwa ikifanya kwa taasisi hizo jijini Dar Es Salaam kuzisaidia kutekeleza majukumu yao.
Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar Es Salaam na Meneja Mawasiliano wa TTCL, Bw. Nicodemus Thom Mushi, alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari (Maelelezo) ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali kwa Taasisi zake kuwasiliana na Umma na kutoa ufafanuzi wa hoja mbali mbali.
“TTCL imejipanga vyema kufanikisha azma hii ya Serikali ya kuhamia Dodoma. Tupo tayari na tunao uwezo mkubwa wa Rasilimali watu, vifaa na utaalamu wa kutosha katika kutoa huduma za Mawasiliano. Tunawahakikishia wateja wetu wote kuwa, watakapochagua kuitumia TTCL, watakuwa wamefanya uchaguzi sahihi. Nitumie fursa hii kuziomba taasisi zote za Umma zinazohamia Dodoma na taasisi zote kwa ujumla kutumia huduma za TTCL ambazo siku zote zimethibitika kuwa ni huduma bora, za uhakika na zenye gharama nafuu,” alisema Bw. Thom Mushi.
Akizungumzia kuhusu mipango ya Kampuni hiyo kuboresha huduma zake, Bw. Mushi alisema, kwa kutumia fursa iliyopo katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, TTCL inaendelea kutekeleza kwa vitendo wajibu wake kwa Umma kwa kuwa mstari wa mbele katika kuunganisha Kampuni, Taasisi, Ofisi za Serikali, Mashirika ya Umma na binafsi wateja waliopo nchi jirani ili waweze kupata Mawasiliano ya uhakika wakati wote.
Kwa sasa tunao Mpango Mkakati wa Biashara wa miaka mitatu(Strategic Business Plan 2016-2018) unaolenga kuboresha na kuleta huduma mpya katika soko, kuongeza jita na uwajibikaji ili kutoa huduma bora kwa Wateja wetu hasa tukizingatia kuwa, TTCL ni mhimili mkuu wa mawasiliano nchini Tanzania.
Akifafanua kuhusu hatua muhimu zilizochukuliwa na TTCL hadi sasa kutekeleza mpango wa mabadiliko, alisema ni pamoja na kuboresha miundombinu ya mtandao wa Simu na Data, kuondoa mitambo chakavu, kuleta huduma bora na zenye kukidhi mahitaji.
Aidha aliongeza kuwa TTCL imeboresha miundombinu ya simu za mezani na Mkononi kwa kuleta teknolojia ya GSM -2G, UMTS-3G na 4G LTE sokoni ili kwenda sambamba na ushindani wa soko la mawasiliano. Teknolojia hii itasaidia kuongeza ufanisi katika kutoa huduma ya simu za mezani, simu za mkononi na huduma ya intaneti yenye kasi zaidi.
“…TTCL inaendelea na juhudi za kuboresha miundombinu ya mawasiliano ya Data nchi nzima (IP Core Network, IP transport Network, Metro Network). Hii itaongeza ubora wa huduma zetu kwa wateja wetu kama vile Wizara, Idara na Taasisi za Umma, Serikali za Mitaa, Taasisi za fedha, Kampuni za Umma na binafsi na wadau wengine wa ndani na nje ya nchi. Kufanikiwa kwa mpango huu kutaleta mabadilko chanya katika huduma za kijamii kama vile Elimu, Afya, Biashara, Uwekezaji, Ujasiriamali, Kilimo, Ufugaji na huduma nyingine ambazo kwa kiasi kikubwa zinahitaji mawasiliano ya uhakika ili kufanyika kwa ufanisi.”
Wakati huo huo, kampuni ya TTCL imempongeza mkurugenzi mpya wa Idara ya Habari (Maelezo) Mwanahabari Mwandamizi, Ndugu Hassan Abbas, kwa kuteuliwa kwake kuwa Mkurugenzi wa Idara hiyo.
“Napenda kuchukua fursa hii kwa niaba ya Menejimenti na wafanyakazi wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kumpongeza Ndugu Hassan Abbas, kwa kuteuliwa kwake kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo.”
“Wasifu wa Ndugu Abbas unatupa imani kubwa kwamba, chini ya uongozi wake, pamoja na utekelezaji wa Majukumu mengine, Idara ya Habari Maelezo itaendelea kutoa mwongozo thabiti kwa Maafisa Habari na Mawasiliano wa Serikali pamoja na kuhakikisha kuwa, Umma unapata taarifa sahihi na kwa wakati muafaka kuhusu utendaji wa Serikali katika kuwatumikia,” alisema Bw. Thom Mushi.