Zaidi ya Wakazi 265 Mbezi Salasala Wanufaika na DAWASCO

  Bomba likitoa maji katika moja ya mitaa ya Salasala jijini Dar es Salaam.

Bomba likitoa maji katika moja ya mitaa ya Salasala jijini Dar es Salaam.

Na Dixon Busagaga

WANANCHI zaidi ya 265 wa mtaa wa Upendo, Mbezi Salasala wilayani Kinondoni
wamelishukuru Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es salaam (DAWASCO), kwa
kuwafikishia huduma ya Majisafi waliyoipatia shida kwa zaidi ya miaka 10
iliyopita.

Akizungumza wakati wa mkutano wa pamoja wa serikali za mitaa na DAWASCO,
Mjumbe wa mtaa wa Upendo Bw. Robert Massawe amepongeza juhudi zilizofanywa na
Dawasco za kuwapatia huduma ya Maji wananchi wa
eneo lake na kwamba juhudi hizo zinaendana na kauli ya serikali ya awamu ya
tano inayosema hapa kazi tu.

Akieleza historia fupi ya eneo hilo Bw. Massawe alisema tangu watu waanze
kuhamia eneo hilo huduma ya Maji ilikuwa ni ya kununua kutoka mtaa mwingine wa
mbali ambao ulikuwa umefikiwa na huduma hiyo ya Maji.

“Ilifikia kipindi gharama ya kununua Maji ni kubwa kuliko gharama ya
chakula, na wananchi wengi walikuwa wakitumia muda wao mwingi kuhangaika
kutafuta Maji jambo ambalo lilikuwa likikwamisha kutekeleza majukumu mengine ya
kujenga nchi” alisema Massawe.

Nae mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Bi. Sofia alisema; “Kweli DAWASCO imemtua
mama ndoo ya Maji kichwani, sisi akina mama ndio tuliokuwa tukiteseka zaidi na
suala la Maji, lakini akina mama wa mtaa huu tulijitoa ili kupambana na janga
la Maji ambalo lilikuwa likitukabili, na hatimaye tumefanikiwa kupata huduma ya
Maji”

Kwa upande wa Dawasco, Meneja wa Mkoa wa Tegeta, Bw. Alpha Ambokile
amewataka wakazi wa mtaa huo kujitokeza kwa wingi kufanya maombi ya kuungiwa
huduma ya Maji kwa kuwa tayari huduma hiyo imefika katika makazi yao, baada ya
kuhangaika kwa muda mrefu wakisaka huduma hiyo, na ameahidi kuwaunganishia
huduma Maji mapema na kwa uharaka zaidi, mara tu baada ya kupokea maombi yao ya
kuungiwa huduma.

“Ninawaomba mjitokeze kwa wingi ili kwa pamoja tuweze kuwaunganishia huduma
ya Maji, nitawatengea siku yenu maalum ambayo timu yangu ya ufundi itakuja
kuwafanyia maunganisho ya Maji, ambao bado hamjafanya maombi, fanyeni haraka
ili tuweze kuwaunganishia wote kwa pamoja huduma ya Maji” alisema Ambokile