Barcelona Wakiona Cha Moto Kwa Liverpool

liver

Sadio Mane aliifungia Liverpool bao lake la kwanza walipowabana vigogo wa Uhispania Barcelona 4-0 katika mechi ya kirafiki huko Wembley.

Mane hakuogopa kuwepo kwa wachezaji nyota wa Barcelona Luis Suarez na Lionel Messi katika mechi hiyo ya kuwania kombe la kimataifa la mabingwa yaani International Champions Cup iliyochezwa katika uwanja wa Wembley.

Mane, aliyenunuliwa katika dirisha la uhamisho kwa kitita cha pauni milioni £34 alifungua kivuno hicho cha mabao kunako dakika ya 15 muda mchache tu kabla ya Javier Mascherano kujifunga mwenyewe.

Mkenya aliyebadili uraia na kuhamia Ubelgiji Divock Origi na Marko Grujic walifunga bao moja kila mmoja.

Mshambulizi wa Uingereza Daniel Sturridge hakushiriki katika mechi hiyo kwa sababu alikuwa anauguza jeraha la paja.
Mkufunzi wa Liverpool Jurgen Klopp alisema kuwa Milner alilazimika kuondoka uwanjani baada ya kujeruhiwa kisigino.

The Reds watafungua kampeini yao ya msimu mpya dhidi ya Arsenal mnamo Agosti tarehe 14 .

Hata hivyo mechi hiyo ya kirafiki iliweka historia kwa kuwa na idadi kubwa ya mashabiki.

Mashabiki 89,945 walifika Wembley kutizama nyota hao wa ligi kuu ya Uhispania
Matokeo Mengine

Mshambulizi wa Uhispania Fernando Llorente alicheza mechi yake ya kwanza tangu ajiunge na Swansea na kuisaidia kuizaba Stade Rennais 1-0 katika uwanja wa Liberty Stadium.
Bao hilo lilitiwa kimiani na Jay Fulton.
Espanyol, 1-0 Everton.
Crystal Palace 3-1 Valencia
Hull 1-2 Torino