Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amekagua barabara ya Makongolosi-Rungwa-Itigi hadi Mkiwa yenye urefu wa jumla ya KM 412 na kuhaidi ujenzi wa kiwango cha lami sehemu ya barabara ya Itigi-Mkiwa yenye urefu wa Km 35.
Akizungumza mara baada ya kukagua barabara hiyo Waziri Prof. Mbarawa amesema Serikali itaijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami ili kufungua fursa za uchumi wa mkoa wa Singida, Tabora na Mbeya.
“Barabara hii imekuwa ya changarawe kwa muda mrefu sasa ni wakati muafaka kujengwa kwa lami ili wananchi wa mikoa hiyo wanufaike na kukuza uchumi wao”, amesema Prof. Mbarawa
Prof. Mbarawa amemtaka Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Singida Eng. Leonard Kapongo kusimamia barabara hiyo kukamilika kwa wakati ili kurahisisha huduma za usafiri kwa wananchi na kuunganisha mikoa hiyo.
Kwa upande wake Meneja wa TANROADS Mkoa wa Singida Eng. Leonard Kapongo amesema katika mkoa wake una jumla ya KM 219 ambapo ujenzi wake utaanza katika sehemu ya Barabara ya Mkiwa hadi itigi KM 35 na kwa upande wa Mkoa wa Mbeya ujenzi utahusisha kipande cha Makongorosi hadi Lupa KM 30 ili kuleta uwiano wa ujenzi wa barabara kwa mikoa hiyo miwili.
“Serikali imetenga fedha za kuanzia utekelezaji wa mradi hivyo tutasimamia ujenzi huo kwa kuzingatia viwango vinavyohitajika na kukamilika kwa wakati ili wananchi waweze kusafirisha bidhaa zao kwa urahisi”, amesisitiza Eng. Kapongo
Naye Mbunge wa Manyoni Magharibi Mhe. Yahya Massawe amesema kuwa barabara hiyo imekuwa haipitiki kipindi cha masika na hivyo ameishukuru Serikali kwa kuipa kipaumbele barabara hiyo kutokana na umuhimu wake kwa mikoa ya Singida, Mbeya na Tabora.
Barabara ya Mkiwa-Itigi KM 35 imeshakamilika kufanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami na katika mwaka wa fedha 2016/2017 kwa kuanzia imetengewa kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 5.8.