Serikali imesema itatumia kiwanda cha Kongolo cha Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) kilichopo Mbeya kuzalisha mataruma yatakayotumika kwenye ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge) inayotarajiwa kuanza kujengwa hivi karibuni ili kupunguza gharama.
Hayo ameyasema Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa alipotembelea kiwanda hicho kuona utendaji kazi na uzalishaji unaopatikana na kuiagiza kamati maalumu ya ujenzi wa reli hiyo kutembelea kiwandani hapo kuangalia uwezo wa uzalishaji wa kiwanda hicho.
Profesa Mbarawa amesema Serikali ina dhamira ya kufufua viwanda hapa nchini ili kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania na kuifikisha nchi katika uchumi wa kati kupitia mapinduzi ya viwanda ifikapo mwaka 2025.
“Nitahakikisha mkandarasi atakeyejenga reli ya hii anatumia mataruma yatakayozalishwa katika kiwanda hiki, badala ya kuagiza vifaa vya ujenzi kutoka nchi za nje”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Ameongeza kuwa kwa kutumia kiwanda hicho Serikali itaokoa pesa ambazo zitaisaidia TAZARA kujiongezea mapato yatakayotokana na matengenezo ya mataruma na kupanua wigo wa kibiashara kwa wateja wa ndani na nje ya nchi.
Aidha, Waziri Prof. Mbarawa amekagua maabara ya kupima viwango na ubora wa kokoto na nondo kilichopo kiwandani hapo na kutoa mwezi mmoja kwa TAZARA kupata cheti cha ukaguzi kutoka Shirika La Viwango (TBS), ili iweze kurasimishwa rasmi.
Kwa upande wake Msimamizi Mkuu wa kuzalisha mataruma katika Kiwanda Cha Kongolo cha TAZARA-Mbeya Eng. Boniface Phiri amesema kuwa fursa ya kuwa sehemu ya mradi wa ujenzi wa reli ya Kisasa itaongeza uzalishaji wa kiwanda na kukuza pato la Mamlaka.
“Kwa kushirikiana na wenzetu tutaongeza vifaa ili tuweze kuzalisha kwa wingi na ubora unaotakiwa katika mradi huu”, amesema Eng. Phiri.
Kiwanda cha Kongolo ni kiwanda pekee katika nchi za Afrika na kati kinachozalisha mataruma kwa ajili ya reli na kina uwezo wa kuzalisha mataruma elfu ishirini na nne kwa mwaka.
Waziri Prof. Mbarawa yupo katika ziara ya kukagua miundombinu ya reli, barabara na mawasiliano mkoani Mbeya.