BENKI ya NMB imezindua mpango mkakati wenye thamani ya mabilioni kwa ajili ya kuboresha huduma zake za fedha kwa miaka mitano. Mpango mkakati huu hususan unahusu kupanua huduma za fedha kwenye mazao zaidi ya kilimo – kutoka matano mpaka zaidi ya 12.
Mpango huu utatoa fursa ya huduma za fedha sio tu kwa wakulima (kupitia mfumo wa vikundi na kwa mkulima mmoja mmoja), lakini vilevile utaongeza uzalishaji zaidi kupitia mnyororo mzima wa thamani katika kilimo – yaani tangu kwa mtoa pembejeo, mzalishaji (mkulima), mchakataji, msafirishaji, mfanya biashara (muuzaji wa jumla, wa rejareja, na wanje ya nchi).
Hivyo NMB imetenga kiashi kisichopungua TZs 500 bilioni kwa ajili ya huduma za fedha kwenye kilimo kwa miaka mitano ijayo. Huduma hii inalenga kuwafaidisha wakulima kuboresha kilimo chao, kuboresha mazao yao, na hivyo kuongeza kipato; na hii itapelekea hata kuongezeka kwa mazao ya kilimo yanayouzwa nje ya nchi.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa NMB, Bi. Ineke Bussemaker, alisema kwamba benki yake inatambua umuhimu na nafasi ya sekta ya kilimo kwenye uchumi wa nchi hii, na ndiyo maana imechukuwa juhudi za makusudi kuboresha na kupanua huduma za fedha zinazolenga kuikuza sekta hii.
“Upatikanaji wa huduma za fedha umekuwa ndiyo kikwazo kikubwa cha ajira kwenye mnyororo wa thamani wa sekta ya kilimo. Mpango na muundo huu mpya tunaouzindua leo utapelekea njia mbadala bunifu katika upatikanaji wa sekta ya kilimo,” alisema Ineke.
Alisisitiza “Kwa kuzingatia umuhimu wa kuboresha sekta ya kilimo Tanzania, tunalenga kujenga mazingira na taratibu ambazo mkulima mdogo na washiriki wote kwenye mnyororo huu wa thamani wataweza kuboresha ufanisi: katika upatikanaji wa pembejeo, uzalishaji kwa njia za kisasa (mbgu bora, mbolea, kutumia zana na nyezo mbalimbali za kilimo na nyinginezo pamoja na ufanisi kwenye masoko. Yote haya yanawezekana kupitia kupatikanaji wa uhakika wa huduma za fedha kwemye kilimo.
“NMB tunaona fursa kubwa sana kwenye sekta ya kilimo”, aliongeza. “Tunaamini kwa kuongeza ushiriki wetu kwenye sekta hii, kutakuwa na msukumo chanya kwenye maisha ya wakulima wetu na wote kwenye mnyororo wa thamani wa sekta hii, na vilevile kutimiza malengo ya NMB”. Alisisitiza.
Bi Bussemaker vilevile alisema kwamba NMB Tayari inawafikia wakulima wadogo wasiopungua 600,000 nchi nzima. Kwenye mpango mkatai huu mpya, benki hii sasa vilevile inawalenga wakulima wakubwa, wafanyabiashara wa pembejeo, wachakataji wa mazao ya kilimo, wafanyabiasha / wauzaji wa mazao na wahusika wengine wote kwenye mnyororo mzima wa thamani katika kilimo.
Katika uzinduzi huu ilitolewa taarifa kwamba, kama sehemu ya NMB katika kuwajibika kwake kwenye jamii (corporate social responsibility), NMB hutoa elimu ya fedha na mafunzo ya biashara kwa watanzania wengi, ikiwa ni pamoja na wakulima. Hii huhusisha kuwajengea uwezo wa namna bora ya kusamamia mapato yao. Kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania. Huchangia 70% wa kipato cha kaya za vijijini. Huajiri 75% ya Watanzania na kuchangia wastani wa 26% ya pato la taifa (GDP).
Asilimia 46% ya ardhi ya Tanzania inafaa kwa uzalishaji wa kilimo; wakati ni 19% tu ya hii inatumika. Sekta hii inakuwa kwa watani wa 4% kwa mwaka, lakini kuna baadhi ya mazao yanakuwa kwa kiwango kikubwa sana kupita mengine, wakati mauzo ya nje kwa baadhi ya mazao yanaongezeka kwa kiasi kikubwa sana. Japo kuna mengi ya kuboresha kwenye sekta hii ya kilimo, kwa kiasi kikubwa mustakabali wake unaonesha matumaini makubwa.
Kuhusu NMB
NMB ni benki kinara na inayoongoza Tanzania, katika idadi ya wateja, na mtandao wa matawi. Ikiwa na matawi zaidi ya 178, NMB inauwakilishi (matawi) kwenye Zaidi ya 95% ya wilaya zote za Tanzania. NMB inahudumia wateja binafsi, wateja wadogo, wa kati na wakubwa / makambpuni. Benki hii inajivunia kumbukumbu nzuri kwenye mahesabu yake ya pesa inayotokana na miaka mingi ya ufanisi ulio bora kibiashara. NMB imeorodheshwa kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam. Rabo Bank ya Uholanzi ni mshiriki wa karibu wa NMB, ambayo imewekeza na kumiliki 34.9% ya hisa za NMB.