Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amezitaka taasisi zilizo chini ya Wizara yake kuanzisha mfumo maalumu wa makubaliano utakaotumika kupima utendaji kazi wa watumishi ili kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa na kutoa matokeo chanya.
Waziri Mbarawa ameyasema hayo Mkoani Rukwa alipofanya mazungumzo na Viongozi na watendaji wa taasisi hizo wakati alipotembelea mkoa huo kwa lengo la kukagua hali ya miundombinu na kuwaeleza mtazamo mpya wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Amesema katika mfumo huo Waziri ataingia mkataba na wenyeviti wa bodi wakati Katibu Mkuu wa kila sekta kuingia mkataba na watendaji wakuu wa taasisi hizo na watendaji hao wataingia mikataba na wafanyakazi wao ili kuweza kuweka mazingira ya kila mfanyakazi kufikia malengo yaliyowekwa na wizara pamoja na taasisi husika.
“Mimi nitawekeana mkataba na wenyeviti wa bodi za taasisi zote, kwa Sumatra moja ya vipengele vitakavyokuwa kwenye mkataba huo ni pamoja na mkakati madhubuti wa kupunguza ajali za barabarani zinazosababisha vifo kwa Watanzania, TCRA Makusanyo kwenye makampuni ya simu na taaasisi nyingine hivyo hivyo”, amesema Prof. Mbarawa.
Aidha, Waziri Mbarawa amehimiza taasisi hizo kufanya kazi kwa bidii ili kuwajengea miundombinu iliyo bora watanzania ili kuweza kuwafikisha katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Aidha, Profesa Mbarawa amewataka watendaji hao kufanya kazi kwa ubunifu, kasi na uadilifu ili kuweza kutatua changamoto zinazowakabili wananchi na kuwajibika kwa ajili ya maslahi ya wananchi na kubadili maisha ya watanzania kwa ujumla.
“Ni wakati wa kutekeleza kauli mbiu ya hapa kazi tu kwa vitendo, hivyo nawataka muwe wabunifu katika utendaji kazi za kila siku na muweze kutoa matokeo chanya ya haraka kwa wananchi”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Awali akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Songwe Lt. Mstaafu Chiku Galawa, Profesa Mbarawa amesema Serikali kupitia wizara yake itaendelea kupandisha hadhi baadhi ya barabara zilizo chini ya Halmashauri na kuwa chini ya Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), ili kuweza kuendelea kuboresha hali ya miundombinu na kuunganisha mkoa huo na Mikoa ya Mbeya, Rukwa pamoja na nchi zinazozunguka mikoa hiyo kwa barabara za lami.
Profesa Mbarawa amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa huyo kuwa Serikali itaendelea kufanya matengenezo kwa barabara zote nchini kupitia gawio kutoka Mfuko wa Barabara nchini (Road fund) ili kuinua uchumi wa Mkoa.
Waziri Mbarawa yupo katika ziara ya kukagua utendaji kazi kwa wafanyakazi pamoja na hali ya Miundombinu katika mikoa ya nyanda za juu kusini.