Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAJUMBE wa Mkutano Mkuu Maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) leo hii wamemchagua Rais John Pombe Magufuli kuwa Mwenyekiti mpya wa chama hicho taifa katika uchaguzi uliofanyika mjini Dodoma. Mkutano huo ulioongozwa na Mwenyekiti mstaafu wa CCM na Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete uliudhuliwa na wajumbe 2,398, ambapo wajumbe wote walimchagua bila kumpinga wala kuharibika kwa kura.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, Dk. Kikwete alisema Mkutano Mkuu Maalum wa CCM ulikuwa na jumla ya wajumbe 2,398. Alisema jumla ya kura zilizopigwa ni 2398 na wote wamepiga kura za ndio kwa Dk. Magufuli. Aliongeza kuwa hakuna kura iliyompinga wala kuharibika. Kwa ushindi huo Dk John Pombe Magufuli ametangazwa kuwa Mwenyekiti mpya wa chama hicho aliyeshinda kwa asilimia 100. Akiwashukuru wajumbe wa Mkutano Mkuu CCM, Rais Dk. Magufuli amewataka kusimama kwa pamoja na kukiimarisha chama ikiwa ni pamoja na kupambana na matukio ya rushwa na ufisadi ili kusimamia haki na pia kuvunja makundi.
“Nimedhamiria kushirikiana na wanachama wenzangu ili kukomesha tabia zote zisizofaa ndani ya chama ikiwa ni pamoja na wale wote watakao toa au kupokea rushwa katika uongozi wangu hatua kali zitachukuliwa hii itasaidia kukomesha tabia zote za usaliti ndani ya chama kwani ni kheri kukaa na mchawi kuliko msaliti,” alisema Dk. Magufuli.
Amewataka wana CCM kuacha kubweteka kwani Watanzania wanataka maendeleo walioyaahidi katika ilani za uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 2015 na kuwafanya waibuke kidedea.
Aidha amewataka wanachama wote wa CCM kujenga chama madhubuti kwa kukemea rushwa na ufisadi kwani wasiokuwa tayari ni kher kujiandaa kuondoka katika nafasi zao. “ Nataka kuona CCM inayoheshimika inayojitegemea sio ombaomba kwa wafadhili kwani tabia hizo ndio zinazosababisha kupoteza majimbo kwani watu wameweka mbele tabia za rushwa,” alisema.
Aidha Dk. Magufuli ameahidi kusimamia maslahi ya wafanyakazi wote wa chama hicho ikiwa ni sambamba na kuimarisha umoja wa Wanawake, Umoja wa vijana Jumuhia ya wazazi ikiwa ni sambamba na kuanzisha kikosi kazi kwa kutambua mali zote za chama ili kusaidia kukusanya mapato ya chama ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya wanachama, wapenzi pia mashabiki wa chama hicho.
Dk. Magufuli alisema CCM haina budi kujipanga upya ikiwa ni sambamba na kupitia upya katiba ya chama, Ilani ya uchaguzi ya chama ikiwa nisambamba na kuondoa mambo ambayo hayana ulazima kama kuwaacha watoto wasome kuliko kuwaweka katika vikundi vya chipukizi pia kuondoa mrundikano wa nyadhifa kwa mtu mmoja zisizo na ulazima.
Amewataka CCM kushirikiana ili kuhakikisha wanatekeleza ilani yao ya uchaguzi waliozitoa wakati wa kampeni ikiwa ni pamoja na elimu bure, afya, maji pamoja na kuwahudumia wazee na wasiojiweza.
Dk. Kiwete akimkabidhi vitendea kazi amemtaka mwenyekiti mpya kuhakikisha ana simamia Ilani ya Chama, Kanuni za Uchaguzi za CCM, Ilani ya Uchaguzi ya CCM hii ikiwa ni sambamba na tathmini ya uchaguzi mkuu uliofanyika oktoba 2015 walioifanya wenyewe ikiwa ni njia ya kugundua mapungufu na mafanikio yaliyopatikana.
Naye mwenyekiti wa chama cha TLP ndugu Augustino Mrema amemshukuru Mwenyekiti huyo mpya kwa kuwa na imani naye kwa kumchagua kuwa kiongozi wa Paroll na kuwaasa wapinzani kuacha tabia za kususa na kuwataka kujipanga upya kwa uchaguzi ujao na kuwatumikia watanzania ambao ndio waliowachagua na kuacha kutoka nje ya bunge kwa visingizio visivyofaa na kupinga kwa mambo harari kuliko kutoka bunge.
Aidha Mwenyekiti wa UDP John Cheyo amewaasa wanasiasa wenzaake kuwa siasa siyo ugomvi na kuwataka kushirikiana ikizingatiwa kuwa hawawezi kuing’oa CCM ikiwa kila mtu atajipanga pekeyake bila kushirikiana kwa pamoja na kuwataka kuacha kuzurura kwa kusema ubaya wa CCM na kero za wananchi kwani ndizo wanazozifanyia kazi CCM kwa sasa.
“Chama cha Mapinduzi ni kigumu kuking’oa madarakani ukishatambua hilo kinahitaji ujue siasa za utu uzima na ukomavu,”
Ameongeza kuwa ni lazima kuonyesha siasa za ukomavu ikiwa ni sambamba na kudumisha Amani na Upendo kwani ndani ya hilo ndipo kwenye siri ya mafanikio kwani siasa za shari hazitawasaidia wala hawatapata nafasi ya kuitawala nchi.
Naye Fred Mpendazoe aliondoka katika cha hicho akitimkia UKAWA amewataka wana CCM kushikamana kwani umoja wao ndio ushindi wao ameona jinsi Dk. Magufuli alivyoamua kupiga umasikini kwa vitendo kitendo ambacho kimemfanya yeye kurudi katika chama chake kwani hakuyaona hayo huko alikotoka.
Mgana Msindai akirudi katika chama chake cha awali ameomba radhi wanachama wote wa CCM kama aliwakwaza pia kuwataka kuendelea kukijenga chama chao kwani ndio njia sahihi na kuwaambia mkutano mkuu kuwa utendaji wa Dk. Magufuli umekuwa kama jongoo kwani tangu ashike wadhifa wa urais amegusa kila eneo bila kujali wala kuonea.