Shirikisho la Muziki Lazungumza na Naibu Waziri Sanaa na Michezo

Katibu Mkuu mpya wa Shirikisho la Muziki Tanzania Bw. John Kitime, Julai 21, 2016, amefanya mazungumzo marefu na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Annastazia Wambura ofisini kwa Naibu Waziri huyo.

katika mazungumzo hayo Katibu Mkuu wa Shirikisho aligusia mambo mbalimbali yakiwemo, sehemu za kufanyia kazi za sanaa ya muziki (kumbi), matatizo ya utekelezaji wa Hakimiliki, ukubwa wa kodi za vifaa vya kazi za muziki,  na mengine mengi ikiwemo kumkabidhi Naibu Waziri tafiti mbalimbali zilizofanywa zilizohusu menejimenti ya tasnia ya muziki.

Mazungumzo haya yaliyochukua zaidi ya saa mbili, yalifikia kwa makubaliano kuwa kutakuwa na ukaribu zaidi kati ya Wizara na viongozi mbalimbali wa sanaa ili kuboresha mazingira ya utendaji wa kazi za sanaa.