SERIKALI imesema ipo katika hatua za mwisho kuanza ujenzi wa barabara ya Njombe-Makete kwa kiwango cha lami yenye urefu wa KM 109.4 inayounganisha mikoa ya Mbeya na Njombe ili kurahisisha huduma ya usafiri wa barabara kwa wakazi wa mikoa hiyo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema hayo mkoani Njombe wakati akiongea na wakazi wa kijiji cha Usalule, kata ya Ulembwe, wilaya ya Wanging’ombe mara baada ya kukagua barabara hiyo.
Profesa Mbarawa amesema kuwa Serikali kwa kutambua umuhimu wa barabara hiyo imetenga kiasi cha sh.bilioni 19 katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
“Tumejipanga na tuna nia dhabiti kuhakikisha barabara hii tutaijenga kwa kiwango cha lami na katika kuharakisha kazi hii tutatafuta makandarasi wawili ili ujenzi huu ukamilike kwa haraka”, amesema Prof. Mbarawa.
Aidha, Waziri Prof. Mbarawa amewataka wananchi kushirikiana na Makandarasi watakapoanza ujenzi huo ili kazi hiyo iweze kukamilika kwa wakati na kulete tija kwa wananchi wa Mikoa ya kanda ya kati.
Amesema kuwa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mkoa wa Njombe upo katika hatua za kutangaza zabuni ili kupata Makandarasi wenye uwezo wa kujenga barabara hiyo kwa kuzingatia viwango kulingana na mkataba.
Naye Meneja wa TANROADS Mkoa wa Njombe Eng. Yusuph Mazana amesema kuwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Njombe-Makaete yenye urefu wa KM 109.4 kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami umekamilika na Mhandisi mshauri M/s Crown Teach Consult Ltd ameshawasilisha taarifa ya usanifu wa kina.
“Tumepokea taarifa ya usanifu wa kina kutoka kwa Mhandisi Mshauri hivyo tunahaidi kusimamia utekelezaji wa mradi huu kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi wa mkoa wa Njombe na mikoa jirani”,amesisitiza Eng. Mazana.
Waziri Prof. Mbarawa ameendelea na ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wizara hiyo Mkoani Njombe.
Imetolewa na kitengo cha Mawasiliano Serikalini ,Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasilino.