World Vision watumia bil 3.6 kuboresha shughuli za kijamii Manyara

Baadhi ya miradi inayowezeshwa na World Vision Tanzania

Na Janeth Mushi, Simanjiro

SHIRIKA la Misaada na Maendeleo ya Jamii ya World Vision Tanzania
limetumia zaidi ya bilioni 3.6 kuboresha shughuli za kilimo, ufugaji na
ujasiriamali kwa wakazi wa tarafa ya Moipo Wilaya ya Simanjiro, mkoani
Manyara kwa kipindi cha miaka 15 iliyopita.

Taarifa hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi wa Udhibiti na Ubora wa shirika hilo, Griffin Zakayo alipokuwa akikabidhi miradi ya
maendeleo iliyokuwa ikisimamiwa na World Vision kwa Umoja wa Vikundi
vya Maendeleo Shambarai (UVIMASHA).

Katika sherehe zilizofanyika eneo la mji mdogo wa Mererani, Mkurugenzi
huyo alisema kiasi hicho cha fedha kilichotolewa na World Vision Australia kiligharamia miradi anuai iliyobuniwa na kuendeshwa na wananchi tangu mwaka 1996.

Baadhi ya miradi iliyohusika katika mpango huo ni pamoja na elimu ya
matumizi bora ya pembejeo za kilimo na uhifadhi wa mazao, ujenzi wa
madarasa na nyumba za walimu, upatikanaji wa maji safi na salama,
ufugaji bora na elimu ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.

Viongozi wa UVIMASHA ambao ndio wenye jukumu la kuendeleza malengo
yaliyokusudiwa pia walipewa elimu ya uongozi na usimamizi wa miradi ya
maendeleo ili kuhakikisha mradi huo unakuwa endelevu.

Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa world Vision Tanzania, Mary Lema
alisema licha ya kukabidhi mradi huo, wataendelea kuutembelea mara kwa
mara kuhakikisha uendeshaji bora na unaozingatia utekelezaji wa lengo
la kuinua na kuboresha maisha ya wananchi vijijini.

Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Khalid Mandya aliyekuwa mgeni rasmi
katika sherehe hizo alisema serikali ya wilaya itafuatilia na
kusimamia kwa karibu shughuli za UVIMASHA kuhakikisha miradi yote
iliyoanzishwa inaendelezwa kwa faida na maendeleo ya wananchi huku
akiwaonya viongozi kutoingiza maslahi binafsi katika miradi iliyopo na
itakayoanzishwa.