Askari apigwa risasi na majambazi Arumeru

PC Prosper akionesha majeraha aliyoyapata baada ya kujeruhiwa kwa risasi na majambazi katika eneo la Denish wilayani Arumeru mkoani Arusha, askari huyo amelazwa katika hospitali ya Selian (Picha na Janeth Mushi)

Na Janeth Mushi, Arumeru

ASKARI wa Jeshi la Polisi namba F 6004, PC Prosper amejeruhiwa vibaya na risasi mapajani na majambazi wakati walipokuwa wanajibizana kwa risasi na majambazi hao. Kaimu Kamanda wa Polisi Arusha, Leonard Paul amesema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 2 usiku eneo la Denish Wilaya ya Arumeru barabara ya vumbi iendayo Arumeru River Lodge.

Alisema katika tukio hilo askari waliokuwa na gari namba T 709 AHY aina ya Nissan Terrano, mali ya Arumeru River Lodge, ambapo walikuwa katika doria ya kawaida ghafla lilitokea gari lenye namba za usajili T 777 AGJ aina ya Toyota Land Cruiser mali ya Kampuni ya Unique Safari, likifuatiwa na gari aina ya Corola lililokuwa na namba T 742 ANV ambalo lilikuwa linawatu wanaohisiwa majambazi.

Alisema gari la askari ghafla lilikuta gogo kubwa limewekwa barabarani ndipo wakaamua kupita pembeni ambapo majambazi hao walianza kuwarushia risasi na gari dogo Corola lilipigwa risasi katika matairi yote ya mbele na gari la askari lilipigwa risasi ubavuni na kumjeruhi askari huyo.

Anasema katika majibizano hayo ya risasi walifanikiwa kumkamata
jambazi sugu mmoja na wengine walikimbia. Jina la jambazi huyo linahifadhiwa kwa sasa ili kukamilisha upelelezi na kuongeza kuwa hata hivyo jambazi hilo lilikuwa likitafutwa Polisi kwa kujihusisha na matukio mbalimbali ya uhalifu, likiwemo la mauaji Karatu pamoja na kukutwa na silaha kinyume cha sheria. Anasema jambazi hilo limetoka gerezani hivi karibuni.