Pinda ataka vyombo vya dola kukagua maghala ya Sukari

Shehena ya Sukari ikipakuliwa kwenye ghala

Na Mwandishi Maalumu

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, amevitaka vyombo vya dola mkoani Mara kufanya ukaguzi katika maghala ya wasambazaji wa sukari ili sukari hiyo ichukuliwe na kuuzwa katika maduka ya reja reja ambayo nayo yatauza kwa bei iliyoelekezwa na Serikali. Waziri Mkuu aliwataka kusimamia suala hilo kwa umakini kwa kuwa wasambazaji hao wamekuwa ni walafi wanaojali maslahi yao zaidi bila kuangalia wananchi wanaumia kiasi gani.

Waziri Mkuu aliyasema hayo Septemba 17, 2011 kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Musoma, ambapo alisema kuwa wafanyabisahara ambao ni wasambazaji wakubwa wa sukari pamoja na wa kati wamekuwa si waaminifu katika biashara zao hali inayosababisha bei ya sukari kupanda kila kunavyokucha.

“Vyombo vya dola fanyeni kazi yenu, ingieni kwenye magodown yao kwa kuwa mnayajua, kagueni na sukari iliyopo itolewe na kuuzwa katika maduka ya rejareja na ikiwezekana hata leseni zao chukueni…hawa wamekuwa ni walafi mno wanaoangalia mifuko yao hivyo hatuwezi tukalikubali hili hata kidogo na kama mtashindwa kulisimamia hili niambieni mimi,” alisema.

Aliwahakikishia wananchi kuwa suala hilo linawezekana kwa kuwa uongozi unawafahamu wafanyabiashara wote wa sukari na akatoa mifano kwa baadhi ya mikoa kama Arusha ambayo imefanya ukaguzi huo na kufanikiwa. Alisema kuwa haoni sababu ya kuwa na uhaba wa sukari kwa kuwa inayozalisha inatosheleza mahitaji hivyo akasema kuwa tatizo hilo linasababishwa na wafanyabiashara wenyewe.

“Hawa wasambazaji wanachukua sukari na matokeo yake hapa nchini wanauza kidogo na nyingine kuisafirisha nchi za nje kwa kutumia njia za panya…hatuwezi kuendelea kuona wananchi wetu wakiumizwa na bei kubwa hivyo kuweni na uvumilivu suala hili linafanyiwa kazi kama nilivyotoa maelekezo,” alisema Waziri Mkuu.

Bei ya sukari hapa nchini imekuwa ikipanda kila kunavyokucha ambapo kwa baadhi ya mikoa bei ya sukari imepanda hadi kufikia sh. 2,600/- kwa kilo moja huku maeneo mengine kama Mkoa wa Mara ikiuzwa kwa sh. 2,500/- hadi 2,400. Awali wakati mfumko wa bei ya sukari ulipoanza, Serikali ilitangaza bei elekezi ambapo kilo moja ilitakiwa kuuzwa kwa sh. 1,700 lakini bei hiyo imekwama kutumika kutokana na uhaba wa bidhaa hiyo.