Na Mwandishi Wetu, Musoma
SERIKALI imesema tayari imemtafuta Mwalimu James Irenge (120) ambaye alimfundisha Baba wa Taifa, Julius Nyerere kipindi anasoma na imeahidi kumsaidia mzee huyo matatizo mbalimbali yanayomkabili.
Kauli hiyo imetolewa Septemba 17, 2011 na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipokuwa akifungua mabweni yanayotumiwa na watoto wenye ulemavu wa ngozi na ulemavu wa macho ya Shule ya Msingi Mwisenge iliyoko Manispaa ya Musoma.
Waziri Pinda alisema lengo la kufika shuleni hapo ni kuona kama shule hiyo ambayo ina mchango mkubwa kwa nchi bado ina heshima, na pia kumtafuta mwalimu aliyemfundisha baba wa taifa Mzee Irenge kwa nia ya kumsaidia.
Alisema kuwa katika kusherehekea miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika ni lazima mambo yenye kumbukumbu kama shule hiyo ambayo ni chimbuko la elimu ya mpigania uhuru huyo yawepo na yawe katika hali nzuri.
Aidha aliwataka kutafakari kwa kina ili kuona shule hiyo wanaifanyia kitu gani hasa katika maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru kwa kuwa huwezi kutaja uhuru bila kumtaja Baba wa Taifa hivyo akasisitiza ni lazima shule hiyo iboreshwe na iwe ya mfano ili kulinda hadhi ya Mwalimu Nyerere.
“Lazima shule hii tuifanye ibebe heshima inayostahili…kama majengo yamechakaa hakuna sababu ya kuendelea nayo, jengeni mapya lakini bila kupoteza uhalisia wa mazingira hasa katika darasa alilosoma Mwalimu kwa kuwa ni moja ya kumbukumbu kubwa…tukae pamoja wakiwemo wabunge na wadau wengine wote ambao ukimtaja Baba wa Taifa ni lazima wawepo ili tuone tunaboreshaje shule hii,” alisema.
“Pamoja na haya, shule hii pia inao walemavu wa kuona na wa ngozi ambao niliwahi kutoa machozi kwa ajili yao wakati wimbi la mauji lilipoibuka na kupoteza walemavu hao kama 40 hivi, kilichonifurahisha ni kuona kuwa ufaulu wa walemavu hawa ni mkubwa nah ii ndo inayotuonesha kuwa wana uwezo mkubwa na wanachohitaji ni msaada tu,” alisema.
Alisema kuwa walemavu wa ngozi ni binadamu kama walivyo wengine na haiwezekani wakabadilishwa kwa namna yoyote na kuwafanya ‘dili’ kama walivyokuwa wakidai wakati wa mauaji yao hivyo akasema serikali itazidi kuwajali walemavu hao na kuwasaidia kwa hali na mali.
“Mwaka 2009 walemavu wa ngozi walikuwa tisa na waliofaulu walikuwa saba na kwa mwaka jana walikuwa saba na walifaulu sita hivyo inanipa picha kuwa uwezo wanao kama walivyo wengine,” alisema.
Mapema, akisoma risala ya shule hiyo kwa Waziri Mkuu, Ofisa Elimu wa Manispaa ya Musoma, Dkt. William Itele alisema mbali na Baba wa Taifa, shule hiyo ni chimbuko la viongozi kadhaa wa kitaifa na kisiasa akiwemo Jaji Joseph Sinde Warioba aliyekuwa Waziri Mkuu awamu ya pili, Bhoke Munanka aliyekuwa Waziri Ofisi ya Rais katika awamu ya kwanza, Joseph Butiku aliyekuwa Katibu ofisi ya rais awamu ya kwanza na Deusdedit Wambura aliyekuwa Katibu Ofisi ya Rais awamu ya kwanza. Waziri Mkuu pia alipata fursa ya kutembelea darasa alilosoma Baba wa Taifa na kuona kitabu cha mahudhurio ambacho kilionesha jina lake.
“Hiki kitabu cha mahudhurio hebu na chenyewe kihifadhiwe katika hali ya ubora zaidi kwani baadaye tunaweza kukiangalia kwa gharama kubwa ikiwa ni sehemu ya utalii,” alisema.