SHULE ya Sekondari Lindi iliyopo Mkoa wa Lindi imeteketea kwa moto. Taarifa za awali kutoka kwa mashuhuda zinasema chanzo cha moto huo ni hitlafu ya umeme iliyosababisha cheche na baadaye kuzuka moto. Hata hivyo Jeshi la Polisi mkoani hapa bado linaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha ajali hiyo ya moto.
Taarifa za watu walioshuhudia zinasema jumla ya vyumba vya madarasa tisa viliteketea kwa moto pamoja na maabara mbili za Kemia na Fizikia za shule hiyo. Majengo mengine yaliyoungua ni vyoo vipya vyenye matundu 24 vilivyojengwa pamoja na mali nyingine zilizokuwa kwenye majengo yaliyoungua.
Kikosi cha zima moto mkoani hapa kilifika kwenye tukio kikiwa na gari linalosadikiwa kuwa la kisasa lakini kilishindwa kulitumia baada ya kugoma kupampu maji kutoka kwenye gari. Mtandao huu ulielezwa kuwa Jeshi la Polisi lililazimika kutumia gari lao maalumu la maji ya kuwasha kuzimia moto ili kuokoa jahazi baada ya kuona zimamoto limeshindwa kusaidia. Cheche za moto inasadikiwa zilianza majira ya saa nne na nusu usiku ambapo zilitolewa taarifa kwa vyombo husika kabla ya moto kukolea.