Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeunda tume maalumu huru ambayo itakuwa na jukumu la kuchunguza ajali ya kuzama kwa meli ya Mv. Spice Islanders iliyopoteza maisha ya mamia ya abiria hivi karibuni.
Taarifa ya kuundwa kwa tume hiyo imetolewa jana mjini hapa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee na kuwataja wajumbe wa tume hiyo rasmi.
Mzee amesema ameunda tume hiyo kwa kutumia uwezo aliopewa chini ya Sheria ya Tume za Uchunguzi Sura ya 33 ya Sheria za Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein-hivyo kuamua kuunda Tume hiyo ya Kuchunguza ajali nzima.
Akifafanua zaidi Mzee amesema kuwa Tume itakuwa na Mwenyekiti, na Katibu huku ikiwa na wajumbe nane, ambao wamepatikana kutoka idara mbalimbali za Tanzania Bara na Visiwani kwa sifa kadhaa kulingana na umuhimu wa tukio.
Akitaja tume nzima Mzee alisema itaongozwa na Jaji Abdulhakim Ameir ambaye ni Mwenyekiti wa Tume na Mwanasheria mzoefu ambae kwa sasa ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar.
Alisema Katibu wa tume hiyo ni Shaaban Ramadhan Abdulla ambaye ni mtaalamu wa Sheria za bahari, ambapo kwa sasa ni Mwanasheria katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar (DPP).
Alisema wajumbe wengine ni, Meja Jenerali S. S Omari, COMDR. Hassan Mussa Mzee, Capt. Abdulla Yussuf Jumbe, Capt. Abdulla Juma Abdulla, Salum Toufiq Ali, Capt. Hatib Katandula na Bi. Mkakili Fauster
Alisema wajumbe wengine ni pamoja na Ali Omar Chengo.
“Meja Jenerali S. S. Omari ni Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Wanamaji katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), COMDR. Hassan Mussa Mzee ni Mkuu wa Kikosi cha KMKM na Capt. Abdulla Yussuf Jumbe ni Nahodha mzoefu wa meli za kitaifa na meli za Kimataifa, ambapo pia aliwahi kuwa nahodha wa Meli ya MV. Mapinduzi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,” alisema katika taarifa hiyo.
Akifafanua sifa na uzoefu wa wajumbe alisema, Capt. Abdulla Juma Abdulla, alikuwa katika Kikosi cha KMKM kwa muda mrefu ambapo sasa ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Idara Maalum za SMZ na Salum Toufiq Ali ni Mwanasheria wa siku nyingi Zanzibar ambae ana uzoefu wa sheria za bahari, ambae kwa sasa ni Mwanasheria wa kampuni ya ZANTEL.
“Capt. Hatibu Katandula ni Mkufunzi katika chuo cha Ubaharia cha Dar es Salaam na Bi. Mkakili Fauster Ngowi ni Wakili wa Serikali Mkuu katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu Tanzania. Ali Omar Chengo aliwahi kuwa mwanajeshi JWTZ na baadae kufanya kazi kwa muda mrefu katika Kikosi cha KMKM kabla ya kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar na Naibu waziri wa Mawasiliano wa SMZ huko nyuma,” alisema.