KIPA raia wa Hispania, Juan Jesus Gonzalez, ametua nchini jana mchana, tayari kabisa kufanya majaribio ya kujiunga na Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC.
Ujio wa kipa huyo unatokana na benchi jipya la ufundi la Azam FC chini ya Zeben Hernandez, ambalo linataka kuongeza nguvu kwenye eneo la langoni ili kutengeneza safu bora ya ulinzi na ushindani wa namba katika nafasi hiyo.
Gonzalez mwenye umbo la urefu aliyepokelewa na Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffar Idd, ataanza rasmi majaribio yake mara baada ya kikosi cha Azam FC kuanza mazoezi ya maandalizi ya msimu mpya (2016-17) kati ya leo Jumatano au Alhamisi.
Akizungumza juu ya ujio wake, Zeben alisema kwa ufupi kuwa eneo la langoni ni sehemu muhimu sana ambalo amepanga kuliongezea nguvu zaidi.
“Nimefurahi sana kufanikiwa kwake kutua hapa, namjua Gonzalez ni kipa mzuri na hili ni jambo muhimu sana kwa Azam FC katika kuboresha eneo hilo, atakuwa hapa kwa majaribio akifanya vizuri tutamchukua,” alisema.
Hii ni mara ya pili kwa Azam FC kumleta kipa Mzungu ndani ya kikosi chake, mwaka 2011 iliwahi kumnasa kipa kutoka nchini Serbia, Obren Cirkovic, ambaye alianza kuwika akiwa na timu ya Yanga.
Chanzo: azamfc.co.tz